Kiongozi Muadhamu: Hujuma ya Marekani Syria ni kosa la kistratijia
(last modified Sun, 09 Apr 2017 16:42:23 GMT )
Apr 09, 2017 16:42 UTC
  • Kiongozi Muadhamu: Hujuma ya Marekani Syria ni kosa la kistratijia

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria hujuma ya hivi karibuni ya Marekani nchini Syria na kusema: "Ni jambo linalotarajiwa kwa Marekani kutenda jinai na kukiuka mambo na kudhulumu na imewahi kuyafanya hayo katika maeneo mengine duniani."

Ayatullah Sayyed Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameyasema hayo leo Jumapili mjini Tehran katika mkutano na makamanda wa ngazi za juu wa Majeshi ya Iran kwa mnasaba wa Nairuzi (mwaka mpya wa Hijria Shamsia). Katika tathmini yake kuhusu hatua ya hivi karibuni ya uvamizi wa kijeshi wa Marekani nchini Syria, Kiongozi Muadhamu ameongeza kuwa: "Kitendo cha Marekani ni kosa la kistratijia na wanakariri makosa waliyoyafanya siku za nyuma."

Ayatullah Khamenei ameongeza kuwa: "Watawala waliotangulia Marekani ndio waliolileta kundi la kigaidi la Daesh (ISIS) na kulisaidia. Wakuu wa sasa wa Marekani vile vile wanaendelea kuimarisha ISIS au makundi mengine kama hayo."

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa, hatari ya makundi hayo itawafikia Wamarekani katika siku za usoni na kuongeza kuwa: "Leo Ulaya imetumbukia katika matatizo kutokana na kosa ililofanya katika kuyapa nguvu makundi ya wakufurishaji na hivi sasa watu wa bara hilo hawana usalama wakiwa nyumbani wala barabarani. Marekani pia inafanya kosa hilo hilo."

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi wa Kiislamu akiwa na makamanda wa kijeshi Iran

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameendelea kusema kuwa,  wananchi na viongozi wa Iran wenye itikadi kwa Mapinduzi ya Kiislamu na ambao wanatawakali na kumtegemea Mwenyezi Mungu hawatalegeza msimamo kutokana na vitisho vya maadui. Iwapo wangekuwa wamelegeza msimamo, leo Iran ingekuwa imedorora na kufilisika kiroho na kiustaarabu.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ambaye pia ni Amri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Iran ameashiria uungaji mkono wa pande zote wa madola ya Magharibi kwa Saddam wakati wa vita vya kulazimishwa vya Iraq dhidi ya Iran na kusema: "Serikali za kinafiki za Ulaya ambazo zinadai kumetumiwa silaha za kemikali Syria, wakati wa vita hivyo vya kulazimishwa zilimpa Saddam shehena kubwa ya silaha za kemikali ili azitumie silaha hizo kuvamia mstari wa mbele wa vita nchini Iran ambapo alizitumia kuhujumu maeneo ya Sardasht na Halabcheh."

Ayatullah Khamenei ameashiria mpango wa adui wa kudhoofisha moyo na motisha wa wananchi, viongozi na vikosi vya ulinzi Iran kwa kuchochea hisia ya 'haiwezekani na hatuwezi' na kusema kuwa, vikosi vya ulinzi vya Iran vinapaswa kutawakali na kumtegemea Mwenyezi Mungu na kujiimarisha siku hadi siku na kwa hima  na ubunifu viweze kuziba pengo la mapungfu yaliyopo na hivyo kujitosheleza.