Iran yalaani mashambulizi ya anga ya Uturuki katika ardhi ya Iraq
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amelaani mashambulizi ya anga ya Uturuki huko Iraq na kuyataja kuwa ni ukiukaji wa mamlaka ya kitaifa na umoja wa ardhi ya Iraq.
Ndege za kivita za Uturuki Jumanne alfajiri ziliyashambulia baadhi ya maeneo ya mji wa Sinjar mkoani Nainava kwa kisingizio cha kuwepo ngome za wapiganaji wa chama cha Kikurdi cha PKK. Watu kadhaa waliuawa katika mashambulizi hayo ya Uturuki.
Bahram Qassemi Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameunga mkono msimamo wa serikali ya Iraq katika uwanja huo ikiwa ni radiamali yake kwa mashambulizi hayo ya anga ya Uturuki katika maeneo ya kandokando mwa mji wa Sinjar huko Iraq. Qassemi amesisitiza pia kuwa kukiuka mamlaka ya kitaifa ya nchi nyinginezo kwa lengo na uhalalishaji wowote ule, ni sawa na kukiuka sheria za kimataifa. Amesema jambo hilo linaweza kuandaa uwanja wa kushtadi machafuko katika eneo la Mashariki ya Kati.