Kashani: Mwamko wa wananchi na jeshi umemaliza njama za adui
Khatibu wa sala ya Ijumaa iliyosaliwa leo hapa mjini Tehran, Ayatullah Muhammad Emami Kashani amesema kuwa, mwamko wa siku zote wa wananchi katika nyanja mbalimbali na pia uwezo wa majeshi ya ulinzi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, umeondoa kila aina ya chokochoko za adui dhidi ya taifa hili.
Aidha khatibu wa sala ya Ijumaa mjini Tehran ameashiria wasi wasi wa madola makubwa ya dunia juu ya majaribio ya makombora ya Iran na kuongeza kuwa, vikosi vya ulinzi vya Iran wakiwemo askari wa baharini, hawatafumbia macho aina yoyote ya njama chafu za adui. Ayatullah Muhammad Emami Kashani amesema kuwa, mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu nchini Iran ni kigezo chema kwa nchi zote za dunia na kwamba mfumo huo unapigania tu kudhamini maslahi na manufaa ya watu wake kinyume na mataifa ya kibeberu yanayopigania kuyanyonya na kuyakoloni mataifa mengine. Aidha amesisitiza kuwa, Iran ya Kiislamu si tishio kwa nchi yoyote ile na kwamba hii leo dunia imefahamu kuwa, taifa la Iran ni taifa la kupigania amani na utulivu na halina nia ya kuvamia au kushambulia nchi nyengine yoyote. Aidha ameashiria namna wananchi wa Iran walivyoshiriki kwa wingi katika uchaguzi wa tarehe 26 Februari na kusema kuwa, kuushiriki zaidi ya asilimia 60 ya wapiga kura, ni jibu kali kwa njama na vitisho vya adui wa Mapinduzi ya Kiislamu. Akizungumzia migogoro katika baadhi ya nchi za eneo hili, Ayatullah Muhammad Emami Kashani amesema, Tehran daima imekuwa ikisisitizia udharura wa kutatuliwa tofauti za nchi za eneo hili kwa njia ya mazungumzo ya kisiasa na si kwa mtutu wa bunduki.