Zaidi ya Wairani milioni 56 wametimiza masharti ya kupiga kura
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i28876-zaidi_ya_wairani_milioni_56_wametimiza_masharti_ya_kupiga_kura
Kamati ya Uchaguzi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imesema Wairani zaidi ya milioni 56 wametimiza masharti yote ya kupiga kura na hivyo wanatazamiwa kushiriki katika uchaguzi ujao wa urais.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 09, 2017 23:17 UTC
  • Zaidi ya Wairani milioni 56 wametimiza masharti ya kupiga kura

Kamati ya Uchaguzi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imesema Wairani zaidi ya milioni 56 wametimiza masharti yote ya kupiga kura na hivyo wanatazamiwa kushiriki katika uchaguzi ujao wa urais.

Ali Asghar Ahmadi, Mkuu wa Kamati ya Uchaguzi ya Wizara ya Mambo Ndani ya Iran amenukuliwa na Shirika la Habari la IRNA akisema kuwa, Wairani milioni 56 laki 4, elfu 10 na 234 wametimiza masharti yote ya kushiriki zoezi la kuwachagua viongozi wao akiwemo rais.

Kadhalika amesema raia wa Iran wanaoishi nje ya nchi wataruhusiwa kushiriki uchaguzi huo kwa kutumia paspoti zao. Katibu wa Kamati ya Uchaguzi ya Iran Ali Pur-Ali Mutlaq, hivi karibuni alisema Wairani wanaoishi nje ya nchi wataweza kupiga kura katika vituo 269 vya upigaji kura vilivyoko katika ofisi 131 za kidiplomasia za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika nchi 102 kote duniani.

Maandalizi ya uchaguzi wa rais nchini Iran

Uchunguzi wa maoni uliofanywa na Kituo cha Utafiti cha Shirika la Utangazaji la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran IRIB hivi karibuni ulioyesha kuwa, takriban asilimia 70.6 ya wananchi wa Iran waliotimiza masharti ya kupiga kura wanatarajiwa kushiriki katika uchaguzi wa 12 wa rais humu nchini.

Uchaguzi wa 12 wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran unatarajiwa kufanyika Ijumaa ya tarehe 19 mwezi huu sambamba na uchaguzi wa tano wa Mabaraza ya Kiislamu ya Miji na Vijiji kote nchini.