Wagombea urais Iran wafanya mdahalo wa tatu na wa mwisho
Wagombea sita wa uchaguzi wa 12 wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, jana jioni walifanya mdahalo wa tatu na wa mwisho ambao ulihusiana na suala la uchumi.
Mdahalo huo umewachuanisha Rais Hassan Rouhani, Makamu wa Kwanza wa Rais, Es'haq Jahangiri, Meya wa Jiji la Tehran, Mohammad Baqer Qalibaf, mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Kuainisha Maslahi ya Jamhuri ya Kiislamu, Mostafa Aqa-Mirsalim, Msimamizi wa Haram ya Imam Ridha AS, Sayyid Ebrahim Raeisi na Makamu wa Zamani wa Rais wa Iran, Mostafa Hashemi-Taba.
Wagombea hao sita katika uchaguzi wa 12 wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wamejadiliana njia za kupambana na magendo ya bidhaa na kupunguza uingizaji bidhaa kutoka nje, kupunguza utegemezi wa nchi kwa pato la mafuta, kustawisha usafirishaji nje bidhaa na kuzuia kuuza mali ghafi, kustawisha uzalishaji wa bidhaa za ndani na kuleta fursa za kudumu za kazi, kutoa ruzuku kwa malengo maalumu na vipaumbele vya kuongeza ukuaji wa uchumi. Kila mmoja wa wagombea hao amepata fursa ya kuwatangazia wananchi sera zake katika mambo hayo.
Katika sehemu ya pili ya mdahalo huo, wagombea hao sita wamepewa fursa ya kutoa majumuisho jumla ya mikakati na mipango yao iwapo watachaguliwa kuongoza serikali. Majumuisho hayo jumla yamejikita katika masuala ya kuimarisha viwanda vya usindikaji bidhaa, kupambana na ufisadi wa kiuchumi, kufanyika marekebisho mfumo wa kodi, vitisho vya kuongezeka matumizi ya fedha taslimu, kuongeza ubora wa utengenezaji magari ya Iran pamoja na kuyatia nguvu mashirika ya elimu za kimsingi.
Uchaguzi wa 12 wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran unatarajiwa kufanyika Ijumaa ijayo ya tarehe 19 Mei 2017 ndani na nje ya Iran.