Rais Rouhani awatumia salamu za Ramadhani viongozi wa nchi za Kiislamu
(last modified Sat, 27 May 2017 06:46:44 GMT )
May 27, 2017 06:46 UTC
  • Rais Rouhani awatumia salamu za Ramadhani viongozi wa nchi za Kiislamu

Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amewatumia salamu za Ramadhani viongozi wa nchi za Kiislamu.

Katika salamu hizo tofauti kwa viongozi wa nchi za Kiislamu, Rais Rouhani amewapa mkono wa baraka kwa mnasaba wa kuanza mwezi huu mtukufu na kuwataka wasimame imara kukabiliana na njama za maadui za kuanzisha migogoro bandia kwa lengo la kuudhofisha ulimwengu wa Kiislamu na kueneza chuki dhidi ya Waislamu.

Ufuatiliaji wa mwezi mwandamo nchini Iran

 

Katika sehemu moja ya salamu zake hizo, Rais Rouhani amesema, ni jambo lisilo na shaka kwamba ni jukumu la viongozi wote, wasomi, maulamaa na wanavyuoni wote wa nchi za Kiislamu kuutumia mwezi huu wa rehema na maghufira ya Mwenyezi Mungu kueneza mafundisho matukufu ya dini ya Kiislamu kwa maneno na kwa vitendo na kuonyesha sura sahihi ya rehema iliyomo ndani ya Uislamu na kukabiliana na njama za maadui wa Uislamu za kuzusha migogoro bandia kwa lengo la kuudhoofisha ulimwengu wa Kiislamu na kueneza chuki dhidi ya Waislamu.

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema: Ni matumaini yangu katika mwezi huu adhimu uliojaa baraka, Waislamu wote watapata kheri na baraka kubwa za Mwenyezi Mungu Mtukufu, na vile vile wataomba msaada wa Dhati Takatifu ya Mwenyezi Mungu na kuongeza juhudi zao katika kushikamana na kuwa kitu kimoja ili kwa njia hiyo waweze kuimarisha amani, utulivu na usalama na kuleta matumaini katika nyoyo za Waislamu wote.

Leo Jumamosi tarehe 27 Mei 2017, ndiyo siku ya kwanza ya mwezi mtukufu wa Ramadhani hapa nchini Iran na katika nchi nyingi za Kiislamu kwa mwaka huu wa 1438 Hijria.