Rouhani: Iran daima imekuwa mstari wa mbele kupambana na ugaidi
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i30434-rouhani_iran_daima_imekuwa_mstari_wa_mbele_kupambana_na_ugaidi
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, tangu baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu hapa nchini, Iran ilikabiliana na wimbi la ugaidi na kupoteza maelfu ya mashahidi, na kwamba daima imekuwa mstari wa mbele kupambana na ugaidi.
(last modified 2026-01-14T08:12:18+00:00 )
Jun 13, 2017 23:49 UTC
  • Rouhani: Iran daima imekuwa mstari wa mbele kupambana na ugaidi

Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, tangu baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu hapa nchini, Iran ilikabiliana na wimbi la ugaidi na kupoteza maelfu ya mashahidi, na kwamba daima imekuwa mstari wa mbele kupambana na ugaidi.

Dakta Rouhani ambaye jana jioni alikuwa akihutubia kikao cha Baraza Kuu la Mapinduzi ya Kiutamaduni  ameashiria mashambulizi ya kigaidi ya tarehe 7 Juni mjini Tehran ambayo yaliua watu 17 na kujeruhi wengine 52 na kusema: Wakati Iran imekuwa mstari wa mbele katika kupambana na ugaidi, madola makubwa na nchi zinazodai kutetea haki za binadamu daima zimekuwa zikiwapa hifadhi magaidi na kuyafadhili makundi yao. 

Rais wa Iran amesema, askari usalama na vyombo vya upelelezi vya Iran vimefanya jitihada kubwa na kufanikiwa kugundua na kuzima harakati nyingi za kigaidi. Ameongeza kuwa, vitendo vya magaidi vya kuua watu wasio na hatia ni kazi ya watu waoga na vinazidisha azma ya wananchi wa Iran ya kutokomeza kabisa makundi hayo ya wahalifu. Amesisitiza kuwa, uhai wa makundi ya kigaidi umefikia mwisho katika eneo la Mashariki ya Kati. 

Rais Rouhani katika kikao cha Baraza Kuu la Mapinduzi ya Kiutamaduni

Rais Rouhani amezungumzia pia matukufu ya usiku wa Lailatul Qadr na sifa za Imam Ali bin Ali Twalib aliyeuawa katika siku hizo kwa kupigwa upanga msikitini na akasema: Mtume Muhammad (saw) alimtaja Ali (as) kuwa ni kugezo cha kupambanua baina ya haki na batili na kwamba, kwa msingi huo katika usiku wa kuamkia tarehe 19 Ramadhani ambao ndani yake Imam Ali bin Abi Twalib alipigwa upanga kichwani, nguzo za uongofu na dini ya Mwenyezi Mungu zilipata pigo na dhoruba kubwa.