Waislamu duniani waungana kuswali na kusherehekea Iddil-Fitri
Leo Waislamu wa maeneo tofauti duniani wanaungana katika swala ya Iddil-Fitri, baada ya kukamilisha mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani kwa siku 30. Hapa Iran swala ya Iddil-Fitri imeswalishwa kitaifa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, hapa mjini Tehran muda mfupi uliopita.
Mataifa mbalimbali ya Kiislamu, nayo yanaungana na Waislamu wengine duniani kuswali na kusherehekea idi hiyo leo Jumatatu. Nchini Pakistan swala ya Iddil-Fitri kitaifa itaswaliwa Islamabad, mji mkuu wa nchi hiyo ambapo kabla ya hapo serikali ya nchi hiyo ilitangaza siku tatu za mapumziko ili kutoa fursa kwa Waislamu.

Hii ni katika hali ambayo polisi ya nchi hiyo imetangaza hali ya hatari kutokana na kuwepo uwezekano wa kutokea mashambulizi ya kigaidi, huku ikiwa imefanikiwa kunasa na kutegua mada kadhaa za miripuko zilizokuwa zimeandaliwa kuwalenga Waislamu katika siku za idi. Nchini Iraq, ofisi ya Ayatullah Sayyid Ali Sistan, marjaa mkubwa wa Waislamu wa Shia nchini humo imetangaza siku ya Jumatatu ya leo kuwa siku ya Iddil-Fitri. Hii ni katika hali ambayo nchi kadhaa kama vile, Saudia, Qatar, Imarati, Bahrain, Kuwait, Palestina, Jordan, Sudan na Misri, zilisherehekea jana sikukuu hiyo.

Aidha hii itakuwa ni mara ya kwanza kwa wakazi wa mji wa Mosul huko Iraq kusherehekea Sikukuu ya Iddil-Fitri baada ya kupita miaka kadhaa. Itakumbukwa kuwa mkoa huo ulikuwa unadhibitiwa na kundi la kigaidi na ukufurishaji la Daesh ambalo lilipiga marufuku Waislamu wa eneo hilo kusherehekea Idul Fitr. Kufuatia mafanikio ya serikali na wananchi wa Iraq ya kuukomboa mkoa huo kutoka katik amakucha ya Daesh, wakazi wa eneo hilo wameonyesha furaha kubwa na kutoa pongezi za dhati kwa jeshi la Iraq kwa kufanikiwa kuwaangamiza wanachama wa genge hilo.