Rouhani: Misimamo mikali na ugaidi ni hatari kwa dunia
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema misimamo mikali na ugaidi ni hatari kubwa kwa eneo la Mashariki ya Kati na dunia nzima.
Rais Rouhani ameyasema hayo leo Jumatano mjini Tehran katika kikao cha baraza la mawaziri na kuongeza kuwa, ushindi wa watu wa Iraq dhidi ya magaidi wa ISIS au Daesh na kukombolewa mji wa Mosul ni harakati yenye kupongezwa. Amesema mataifa yote yanapaswa kushirikiana ili kukabiliana na ugaidi kwa njia za kijeshi, kiutamaduni, kisiasa na kiuchumi.
Rais Rouhani amesema Iran ilikuwa nchi ya kwanza kuipa msaada Iraq kwa ajili ya kukabiliana na ugaidi wa ISIS na kuongeza kuwa: "Baadhi ya nchi za eneo hili na dunia zilikasirishwa na hatua ya Iran kuisaidia Iraq, lakini baada ya kuenea ugaidi zilielewa kuwa, Iran iliona mbele wakati ilipoamua kusaidia Iraq katika vita dhidi ya ISIS.
Rais Rouhani aidha amesema, Iran imeonyesha kuwa ni nchi yenye kufuata mantiki katika masuala yote ikiwemo kadhia ya nyuklia. Amesema Marekani imekuwa ikikiuka utekelezaji majukumu yake na kuongeza kuwa, hivi sasa ni vigumu kwa Marekani kuchukua hatua zozote dhidi ya Iran katika uga wa kimataifa.
Rais Rouhani pia ameashiria matamshi ya uingiliaji kati yaliyotolewa na Waziri wa Ulinzi wa Marekani na kusema: "Nchi ambayo katika miongo minne imekuwa ikitafakari kila siku kuchukua hatua za kijeshi dhidi ya Iran imekuwa ikifeli na itaendelea kufeli pia."
Rais wa Iran alikuwa akijibu matamshi ya Waziri wa Ulinzi wa Marekani, James Mattis ambaye hivi karibuni alisema Marekani inapanga kuuangusha mfumo wa Kiislamu unaotawala nchini Iran.