Salehi: Machaguo yote yako mezani endapo Marekani itakiuka JCPOA
(last modified Tue, 08 Aug 2017 14:49:43 GMT )
Aug 08, 2017 14:49 UTC
  • Salehi: Machaguo yote yako mezani endapo Marekani itakiuka JCPOA

Mkuu wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran (AEOI) Ali Akbar Salehi amesema Tehran itaweka machaguo yote mezani endapo Marekani itakiuka makubaliano ya nyuklia ya mwaka 2015 yaliyosainiwa kati ya Jamhuri ya Kiislamu na nchi zinazounda kundi la 5+1.

Dakta Salehi, ambaye pia ni Makamu wa Rais wa Iran ameyasema hayo kwenye mahojiano na kanali ya televisheni ya al-Mayadeen ya Lebanon yaliyorushwa hewani leo ambapo amesisitiza kuwa Marekani ndiyo itakayodhurika zaidi endapo itayakiuka makubaliano hayo yanayojulikana kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA).

Amefafanua kuwa endapo Marekani itahalifu makubaliano hayo ndiyo itakayobeba dhima ya hatua yake hiyo.

Ameongeza kuwa Iran itachukua hatua mkabala kulingana na muelekeo wa Washington kuhusiana na makubaliano hayo.

Iran na nchi zinazounda kundi la 5+1 ziliposaini makubaliano ya JCPOA mwaka 2015 mjini Vienna, Austria

Mkuu wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran amebainisha kuwa, kwa kuzingatia kuidhinishwa makubaliano ya JCPOA na Umoja wa Ulaya, China na Russia, endapo Marekani itajiondoa kwenye makubaliano hayo haitoathiri kuendelea kuwepo kwake.

Mkuu wa AEOI amesema shughuli za nyuklia za Iran zinaendelea vizuri zaidi hivi sasa kuliko ilivyokuwa huko nyuma na akasisitiza kwamba endapo Marekani itakiuka makubaliano ya nyuklia ya JCPOA machaguo yote ya Iran yatakuwa mezani; na Tehran itatoa jibu kulingana na muamala utakaoonyeshwa na Washington kuhusiana na makubaliano hayo.

Makubaliano ya JCPOA yaliyosainiwa kati ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na nchi sita zinazounda kundi la 5+1 ambazo ni Russia, China, Uingereza, Ufaransa, Marekani na Ujerumani yalianza kutekelezwa Januari mwaka 2016, lakini Marekani ambayo ni moja ya nchi zinazounda kundi hilo imekuwa ikikiuka kila mara makubaliano ya JCPOA.

Dakta Ali Akbar Salehi aidha ameuelezea uhusiano wa Iran na Russia kuwa ni imara zaidi hivi sasa kuliko wakati wowote ule na kubainisha kuwa Tehran na Moscow hivi sasa zinajadili miradi kadhaa ya pamoja ukiwemo wa kujenga vinu viwili vipya vikubwa na vya kisasa vya nyuklia katika mji wa Bushehr kusini mwa Iran.../

 

Tags