Ugiriki: Iran ni taifa linaloimarisha amani na usalama Mashariki ya Kati
Waziri wa Mambo ya Ndani nchini Ugiriki amesema kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni nchi muhimu ambayo inafanya juhudi kubwa za kuimarisha amani na usalama katika eneo la Mashariki ya kati.
Panagiotis Kouroumblis, ameyasema hayo alipokutana na Majid Motallebi Shabestari, balozi wa Jamhuri ya Kiislamu nchini Ugiriki, mjini Athens na huku akiashiria ustaarabu wa kale wa Iran amesema kuwa, Iran ni nchi kubwa yenye uchumi na ustaarabu mkongwe na inajulikana kwa kupigania kwake usalama na utulivu katika eneo hili. Kouroumblis Ameashiria historia kongwe ya uhusiano wa nchi hizi mbili na kusema, Iran na Ugiriki ni nchi zenye historia ndefu na yenye uhusiano wa pamoja. Aidha ametaka kuendelezwa zaidi uhusiano wa nchi mbili hizi ikiwemo kustafidi na uzoefu ilio nao Tehran katika nyanja tofauti. Kwa upande wake Majid Motallebi Shabestari, balozi wa Iran nchini Ugiriki amesisitizia udharura wa kuimarishwa ustawi wa kiushirikiano wa pande mbili katika nyuga za kisiasa na kiuchumi baina ya Athens na Tehran. Amesema kuwa, uhusiano wa nchi mbili umekuwa mzuri katika vipindi vya miongo kadhaa iliyopita ambapo viongozi wa nchi mbili hizi wamekuwa wakitembeleana ikiwa ni pamoja na safari ya Waziri Mkuu wa Ugiriki Alexis Tsipras hapa nchini Iran.