Wairani waandamana kupinga mauaji ya Waislamu nchini Myanmar
(last modified Fri, 08 Sep 2017 17:05:38 GMT )
Sep 08, 2017 17:05 UTC
  • Wairani waandamana kupinga mauaji ya Waislamu nchini Myanmar

maelfu ya Wairani waliohudhuria ibada ya Swala ya Ijumaa kote hapa nchini leo wamefanya maandamo katika miji mbalimbali wakipinga na kulaani mauaji yanayoendelea kufanywa na jeshi na Mabudha wa Myanmar dhidi ya Waislamu nchini humo.

Washiriki katika maandamano hayo wametoa taarifa mbalimbali zilizolaani kimya cha jamii ya kimataifa na nchi zinazodai kutetea haki za binadamu mbele ya jinai na mauaji yanayofanywa dhidi ya Waislamu nchini Myanmar.

Vilevile wamewataka viongozi wa nchi za Waislamu na wanazuoni wa Kiislamu kuchukua hatua za kivitendo za kukomesha mauaji yanayofanywa dhidi ya Waislamu wasio na ulinzi nchini Myanmar. 

Taarifa ya wanaandamanaji wakati wa Swala ya Ijumaa ya Tehran imesema kuwa jinai na ukatili unaofanywa dhidi ya Waislamu wa Myanmar ni sehemu ya siasa za ubeberu wa kimataifa na ni jinai dhidi ya binadamu.

Waandamanaji hao pia wameashiria kimya cha nchi kubwa duniani hususan Marekani mbele ya mauaji hayo na kusisitiza kuwa, sera hizo hazitaweza kuzuia wimbi la mwamko wa Kiislamu na kuenea kwa dini tukufu ya Uislamu katika pembe mbalimbali za dunia. 

Maelfu ya Waislamu wameuawa na wengine wengi wamelazimika kukimbilia katika nchi jirani huko Myanmar kutokana na ukatili wa jeshi la serikali na Mabudha wenye fikra za kuchupa mipaka. Makazi na vijiji vya Waislamu hao pia vinateketezwa kwa moto.