Iran: Kujitenga Kurdistan na Iraq kutalipa nguvu Daesh na Israel
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i35093-iran_kujitenga_kurdistan_na_iraq_kutalipa_nguvu_daesh_na_israel
Hussein Amir-Abdullahian, Mkurugenzi Mkuu wa Masuala ya Kimataifa ya Bunge la Iran amesema hatua ya Massoud Barzani, Rais wa Serikali ya Eneo la Kurdistan ya kushinikiza kujitenga eneo hilo na serikali kuu ya Iraq ni sawa na kulishajiisha kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh na kutumikia maslahi ya utawala wa Kizayuni wa Israel.
(last modified 2026-03-03T12:46:59+00:00 )
Oct 01, 2017 11:56 UTC
  • Iran: Kujitenga Kurdistan na Iraq kutalipa nguvu Daesh na Israel

Hussein Amir-Abdullahian, Mkurugenzi Mkuu wa Masuala ya Kimataifa ya Bunge la Iran amesema hatua ya Massoud Barzani, Rais wa Serikali ya Eneo la Kurdistan ya kushinikiza kujitenga eneo hilo na serikali kuu ya Iraq ni sawa na kulishajiisha kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh na kutumikia maslahi ya utawala wa Kizayuni wa Israel.

Amesema jitihada hizo za Barzani hazitakuwa na matokeo mengine ghairi ya kuzipa nguvu Daesh na Israel, hatua ambayo itasababisha ukosefu wa uthabiti katika eneo la Mashariki ya Kati.

Abdullahian ambaye amewahi kuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran katika masuala ya nchi za Kiarabu na Afrika amebainisha kuwa, Wakurdi wa Iraq hawawezi kupata uungaji mkono wala ufanisi wowote kwa kupania kuvuruga umoja wa kitaifa wa nchi hiyo ya Kiarabu.

Massoud Barzani, Rais wa Serikali ya Eneo la Kurdistan la Iraq

Kauli hii inajiri siku chache baada ya Ali Akbar Velayati, Mshauri Mwandamizi wa Kiongizi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika masuala ya kimataifa kumtaja Barzani kama dalali, anayetumikia maslahi ya utawala wa Kizayuni wa Israel.

Licha ya kupingwa vikali kieneo na kimataifa na licha ya serikali kuu ya Iraq kupiga marufuku kura hiyo, lakini tarehe 25 mwezi ulioisha wa Septemba, viongozi wa eneo la Kurdistan la Iraq waliitisha kura ya maoni ya kujitenga eneo hilo na maeneo mengine ya nchi hiyo kwa sababu zao binafsi.

Matokeo rasmi ya kura hiyo yanaonyesha kuwa, asilimia 92.73 ya wapiga kura waliunga mkono kujitenga Kurdistan na Iraq. Asilimia 72.61 ya wakaazi wa eneo hilo waliotimiza masharti walishiriki zoezi hilo.