Iran yaomboleza kifo cha Jalal Talabani, rais wa zamani wa Iraq
Balozi wa Iran mjini Baghdad, Iraj Masjedi ametuma salamu za rambirambi kwa Rais wa Iraq, Fuad Masoum kufutia kifo cha rais wa zamani wa nchi hiyo ya Kiarabu, Jalal Talabani.
Katika ujumbe wake kwa Rais wa Iraq, Balozi wa Iran amesema: "Talabani alikuwa shakhsia ambaye alipambana kwa miaka mingi dhidi ya utawala wa kidikteta wa Ba'ath. Alipokuwa rais wa Iraq, alifanya jitihada chungu nzima kuhakikisha kuwa Baghdad inaimarisha uhusiano wake na nchi za eneo."
Aidha Balozi wa Iran mjini Baghdad ameongeza katika ujumbe huo kuwa, Jalal Talabani alitaka kuona mipaka ya Iraq inalindwa sanjari na kudumishwa umoja na mshikamano wa Wairaqi wote pasina kujali makabila yao.
Mwanadiplomasia huyo wa Iran amemalizia ujumbe huo kwa kuipa pole na kuitakia kila la kheri familia ya Talabani wakati huu inapoomboleza kifo cha mpendwa wao.
Jalal Talabani aliyekuwa na umri wa miaka 83, amefariki dunia akipokea matibabu katika hospitali moja mjini Berlin, Ujerumani baada ya kupatwa na kiharusi.