Mar 22, 2016 03:37 UTC
  • Rais Rouhani asisitiza kutekelezwa sera za Uchumi wa Muqawama

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kuwa serikali yake itatekeleza sera za Uchumi wa Muqawama.

Rais Hassan Rouhani ameyasema hayo katika safari yake kisiwani Kish huko kusini mwa Iran ya kukagua mradi wa matengenezo na uboreshaji wa ukanda wa pwani ya magharibi ya kisiwa hicho.

Rais Rouhani amefafanua kuwa kikao cha wakuu wa maeneo huru ya biashara ya Iran kitakachofanyika leo katika kisiwa cha Hendurabi kilichoko kwenye Ghuba ya Uajemi kitajadili pamoja na mambo mengine hatua zilizochukuliwa kulingana na kifungu cha 11 cha sera za Uchumi za Muqawama.

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kifungu cha 11 cha sera za Uchumi wa Muqawama kinahusu maeneo huru ya biashara na mchango wao katika kuimarisha msingi wa uchumi wa Iran kwa kuvutia teknolojia, mitaji ya uwekezaji na kufanya jitihada katika nyanja za uzalishaji na usafirishaji bidhaa nje ya nchi.

Dakta Rouhani ameongeza kuwa kikao hicho cha leo cha wakuu wa maeneo huru ya biashara ya Iran kitajadili na kukamilisha mipango ya kuharakisha utekelezaji wa kifungu cha 11 cha sera za Uchumi wa Muqawama.

Katika safari yake hiyo kisiwani Kish Rais Rouhani leo anatazamiwa kukagua pia mradi wa uzinduzi wa kinu cha uzalishaji umeme na maji kisiwani humo.../

Tags