Salehi: Marekani inafanya njama za kufuta makubaliano ya JCPOA
Mkuu wa Taasisi ya Nishati ya Nyuklia ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kuwa Marekani inataka kuyasambaratisha makubaliano ya nyuklia ya JCPOA kwa gharama za Iran.
Ali Akbar Salehi amesema Marekani haiaminiki na kwamba misimamo ya viongozi wa nchi hiyo kuhusu makubaliano hayo si sahihi. Mkuu wa Taasisi ya Nishati ya Nyuklia ya Iran ameshiria hatua ya Rais Donald Trump wa Marekani ya kukataa kutangaza kuwa Iran imetekeleza majukumu yake kuhusu makubaliano ya JCPOA na kueleza kuwa, hatua za hivi karibuni za kiongozi huyo zinakiuka makubaliano hayo.
Salehi ameongeza kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itatoa majibu yanayostahili katika uwanja huo.
Amesisitiza kuwa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) ndio marejeo pekee ya kufuatilia masuala mbalimbali ya nyuklia na kwamba Yukia Amano Mkurugenzi Mkuu wa wakalal huo ana jukumu maalumu kwa kuzingatia mwenendo wa Marekani mkabala na makubaliano ya JCPOA.
Rais Donald Trump wa Marekani tarehe 13 mwezi huu alisema kuwa hatothibitisha kuwa Iran imefungamana na kutekeleza majukumu yake kuhusiana na makubaliano hayo ya nyuklia na amepuuza ripoti nane zilizotolewa na wakala wa IAEA ambazo zimesisitiza kuwa Iran imetekeleza majukumu yake kuhusu makubaliano ya JCPOA.