Dec 04, 2017 02:39 UTC
  • Larijani awasili Moscow kushiriki Mkutano wa Kimataifa wa Kupambana na Mihadarati

Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran (Bunge) amewasili Moscow mji mkuu wa Russia akiongoza ujumbe wa ngazi ya juu kwa ajili ya kushiriki katika Mkutano wa Kimataifa wa Kupambana na Mihadarati utakaojadili suala la vita dhidi ya madawa ya kulevya.

Dakta Ali Larijani alisema jana kabla ya kuanza safari yake hiyo ya siku mbili nchini Russia kuwa: Ziara yake mjini Moscow inafanyika lengo likiwa ni kushiriki Mkutano wa Kimataifa wa Kupambana na Mihadarati; ambapo pambizoni mwa kikao hicho Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran atakuwa  na mazungumzo ya pande mbili pia na viongozi wa ngazi ya juu wa Russia.

Dakta Larijani ameongeza kuwa, suala la mihadarati ni kadhia yenye umuhimu mkubwa kwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Russia na kwamba hali ya Afghanistan imebadilika kiasi kwamba uzalishaji wa madawa ya kulevya nchini humo umeongezeka; huku mbinu zinazodaiwa kutumiwa na Muungano wa Kijeshi wa Nchi za Magharibi (Nato) katika kukabiliana na suala hilo zikishindwa kutekelezwa kivitendo. 

Uzalishaji wa dawa za kulevya nchini Afghanistan umeongezeka 

Mkutano wa Kimataifa wa Kupambana na Mihadarati unafanyika leo Jumatatu mjini Moscow kwa kuhudhuriwa na maspika wa mabunge  wa nchi zaidi ya 40 duniani ikiwemo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. 

Tags