Rais Rouhani: Marekani haiwezi kubatilisha mapatano ya nyuklia ya JCPOA
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i37821-rais_rouhani_marekani_haiwezi_kubatilisha_mapatano_ya_nyuklia_ya_jcpoa
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema tokea yaanze kutekelezwa mapatano ya nyuklia ya Iran yanayojulikana kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezwaji, JCPOA, Marekani imetaka mara kadhaa mapatano hayo yabatilishwa lakini haiwezi kufanikiwa katika hilo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 19, 2017 10:39 UTC
  • Rais Rouhani: Marekani haiwezi kubatilisha mapatano ya nyuklia ya JCPOA

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema tokea yaanze kutekelezwa mapatano ya nyuklia ya Iran yanayojulikana kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezwaji, JCPOA, Marekani imetaka mara kadhaa mapatano hayo yabatilishwa lakini haiwezi kufanikiwa katika hilo.

Rais Hassan Rouhani ameyasema hayo leo Jumanne mjini Tehran katika kikao cha kwanza cha kitaifa cha "Ripoti ya Utekelezwaji Haki za Raia" na kuongeza kuwa, iwapo kuna nchi inayopinga JCPOA basi isimtegemee Rais Donald Trump wa Marekani kwani hawezi kufanya lolote.

Rais wa Iran amesisitiza kuwa, mapatano ya JCPOA yatabakia na Iran itaendelea katika mkondo wake.

Mwezi wa Oktoba Trump alikataa kuidhinisha kufungamana Iran na mapatano ya JCPOA yaliyofikiwa mwaka 2015 baina ya Iran na madola sita makubwa duniani ambayo ni Marekani yenyewe, Ufaransa, Uingereza, Russia, China na Ujerumani.

Rais Trump wa Marekani

Kufuatia uamuzi huo wa Trump, Bunge la Kongresi la Marekani lilipewa siku sitini kuamua kuhusu kuwekewa Iran vikwazo vipya lakini baada ya muhula huo kupita bunge hilo halikuchukua uamuzi wowote na sasa mpira umerejeshwa katika uwanja wa Trump.

Kwa mujibu wa sheria ifikapo kati kati ya Januari mwaka 2018, Trump anapaswa kuamua iwapo ataacha kuendelea kutekeleza vikwazo vya nyuklia dhidi ya Iran au la.

Iran imesisitiza kuwa maadamu wote waliofikia mapatano ya JCPOA wanafungamana nayo, basi itaendelea kufungamana na mapatnao hayo ya nyuklia lakini iwapo Marekani itajiondoa katika Mapatano hayo, Iran nayo itachukua hatua mkabala wake.