Askofu wa Waarmenia Tehran: Wakristo hawaitambui Israel
Askofu wa Kanisa la Armenia mjini Tehran amesisitiza kuwa, Wakristo hawatambui serikali inayojiita Israel.
Askofu Sebouh Sarkissian, Mkuu wa Kanisa la Armenia mjini Tehran aliyasema hayo Jumatatu mjini Tehran wakati alipokutana na Bi.Zahra Nejadbahram mwanachama wa Baraza la Kiislamu la Mji wa Tehran na kuongeza kuwa: "Wakristo wako katika sherehe za kukumbuka kuzaliwa Nabii Issa Masih AS (Yesu) katika hali ambayo leo hakuna usalama katika eneo la Beit Lahm kusini mwa Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan, sehemu alikozaliwa Nabii Issa AS". Jana tarehe 25 Disemba ilikuwa siku ya Krismasi ambapo Wakristo hukumbuka kuzaliwa Nabii Issa Masih AS.
Askofu wa Waarmenia mjini Tehran amelaani hatua ya hivi karibuni ya Rais Donald Trump wa Marekani kutambua Quds Tukufu (Jerusalem) kuwa eti ni mji mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel na kusema uamuzi huo hauwezi kukubalika.
Askofu Sarkissian ameongeza kuwa uamuzi wa Trump si tu kuwa ni dhidi ya Palestina na Waislamu bali pia ni dhidi ya ubinadamu.
Kwa upande wake, Bi.Zahra Nejadbahram amesema kuwa, katika kipindi chote cha historia Iran imekuwa mwenyeji wa dini na madhehebu mbali mbali na nukta hii inaonyesha kuwa Wairani wanaishi pamoja kwa amani,urafiki na maelewano pasina kujali dini au madhehebu.