Rais Rouhani: Nchi za Kiislamu zisiwe tegemezi kwa madola ya kigeni
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i39039-rais_rouhani_nchi_za_kiislamu_zisiwe_tegemezi_kwa_madola_ya_kigeni
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema mapema leo katika mkutano wa 13 wa Umoja wa Mabunge ya Nchi za Kiislamu wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) unaofanyika mjini Tehran kwamba njia ya kukabiliana na changamoto za Ulimwengu wa Kiislamu ni kutoyategemea madola ya kigeni.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 16, 2018 05:19 UTC
  • Rais Rouhani: Nchi za Kiislamu zisiwe tegemezi kwa madola ya kigeni

Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema mapema leo katika mkutano wa 13 wa Umoja wa Mabunge ya Nchi za Kiislamu wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) unaofanyika mjini Tehran kwamba njia ya kukabiliana na changamoto za Ulimwengu wa Kiislamu ni kutoyategemea madola ya kigeni.

Rais Rouhani amesema katika mkutano huo wa siku mbili unaohudhuriwa na nchi 41 za Kiislamu kwamba, Iran mbali na kuheshimu ardhi na mamlaka ya kisiasa ya nchi zote inatambua njia ya kutatua kikamilifu matatizo ya Umma wa Kiislamu kuwa ni mshikamano na ushirikiano wa nchi zote za Waislamu. 

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameashiria kuwa baadhi ya nchi zinazusha migawanyiko katika Umma kwa kuchochewa na Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel na kusema kuwa: Sababu kuu ya kuvurugika amani na usalama wa eneo la Mashariki ya Kati na kuendelea kukaliwa kwa mabavu ardhi za Palestina ni uungaji mkono wa hali na mali wa Marekani kwa utawala wa Kizayuni wa Israel na hatimaye kulinyima taifa la Palestina haki yake ya kimsingi ya kuunda dola huru la Palestina mji wake mkuu ukiwa Quds tukufu.

Mkutano wa mabunge ya Kiislamu

Rais Rouhani pia ameashiria kuangamizwa kundi la kigaidi la Daesh na mchango na nafasi ya Iran katika mapambano dhidi ya kundi hilo la kitakfiri na kusema: Moja kati ya matunda ya kushindwa kundi hilo lenye misimamo ya kuchupa mipaka la Daesh ni kurejea tena maudhui ya Palestina katika nafasi yake kuu na kama kipaumbele cha kwanza katika kazi za kisiasa za Umma wa Kiislamu.

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu amesema anatarajia kuwa Umma wa Kiislamu na serikali za nchi za Waislamu kamwe hazitaisahau Quds kama kibla cha kwanza cha Waislamu. Amesisitiza udharura wa kuwa na lengo moja na kujiepusha na mifarakano na kusema kuwa Iran itazidisha jitihada za kuhakikisha Wapalestina wanarejea katika ardhi yao na kuunda dola huru katika ardhi yote ya Palestina mji mkuu wake ukiwa Quds tukufu.

Maspika wa mabunge ya Kiislamu wakutana mjini Tehran

Amesema Iran imejenga uhusiano wake na nchi za Kiislamu kwa msingi wa upendo na udugu wa Kiislamu na kuongeza kuwa: Tehran haiitambui nchi yoyote ya Waislamu kuwa ni mpinzani wake na inaamini kuwa, inawezekana kuzungumza na kushirikiana na hata nchi ambazo inahitilafiana nazo kimitazamo.