Iran haijadiliani na yeyote kuhusu uwezo wake wa ulinzi
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i39379-iran_haijadiliani_na_yeyote_kuhusu_uwezo_wake_wa_ulinzi
Msemaji wa serikali ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, uwezo wa kujihami wa Iran hauwezi kufanyiwa mazungumzo. Ameongeza kuwa, "hakuna yeyote mwenye idhini ya kuingilia masuala ya kujihami na ya makombora ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran."
(last modified 2026-08-17T09:53:57+00:00 )
Jan 23, 2018 11:30 UTC
  • Iran haijadiliani na yeyote kuhusu uwezo wake wa ulinzi

Msemaji wa serikali ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, uwezo wa kujihami wa Iran hauwezi kufanyiwa mazungumzo. Ameongeza kuwa, "hakuna yeyote mwenye idhini ya kuingilia masuala ya kujihami na ya makombora ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran."

Mohammad Baqer Noubakht Msemaji wa Serikali ya Iran ametoa kauli hiyo katika kujibu matamshi ya hivi karibuni ya Jean-Yves Le Drian Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa ambaye amedai kwamba kumeanza mazungumzo na Iran kuhusu mpango wa makombora ya kujihami. Noubakht amesema, "Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haifanyi na wala haitafanya mazungumzo na yeyote kuhusu masuala ya makombora yake."

Msemaji wa Serikali ya Iran amesisitiza kuwa, kuimarisha uwezo wa kujihami ni haki ya kimsingi na isiyopingika ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Wakuu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wamesisitiza mara kadhaa kuwa, miradi ya kujihami ya Iran inayojumuisha makombora ni mstari mwekundu wa nchi hii. Iran inasisitiza kuwa sera zake za ulinzi ikiwemo makombora ni kwa ajili ya kuilinda nchi na kusaidia kudumisha amani, utulivu na usalama katika eneo la Mashariki ya Kati.

Makombora ya Iran yakifanyiwa majaribio

Marekani na baadhi ya waitifaki wake wanataka Iran isitishe miradi yake ya kutengeneza makombora ya kujihami.

Marekani na waitifaki wake wamekuwa wakidai kuwa hatua ya Iran ya kufanyia majaribio makombora yake ni kinyume cha azimio 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Hii ni katika hali ambayo, Nabila Massrali Msemaji wa Mkuu wa Sera za Kigeni katika Umoja wa Ulaya amenukuliwa akisema majaribio ya makombora ya Iran si kinyume cha mapatano ya nyuklia yajulikanayo kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezwaji (JCPOA).