Tehran yamwadhibu jasusi wa Israel katika masuala ya nyuklia ya Iran
-
Abbas Jafari Dolatabadi, Mwendesha Mashtaka wa Mahakama ya Mapinduzi ya Tehran
Mwendesha Mashtaka wa Mahakama ya Mapinduzi ya Tehran amesema kuwa, jasusi mmoja amepatikana na hatia ya kuyafanyia ujasusi madola ya kigeni katika masuala ya nyuklia ya Iran na kuhukumiwa kifungo jela humu nchini.
Kwa mujibu wa shirika la habari la IRIB, Abbas Jafari Dolatabadi, Mwendesha Mashtaka wa Mahakama ya Mapinduzi ya Tehran amesema hayo leo Jumatatu katika kikao cha 25 cha Baraza la Wakuu wa Mahakama za Tehran.

Ameongeza kuwa, mtuhumiwa huyo ambaye hakumtaja jina lake alikuwa na mawasiliano na mashirika ya kijasusi ya madola ya kigeni likiwemo la utawala wa Kizayuni wa Israel. Amesema, jasusi huyo ameonana kwa uchache mara 14 na maafisa wa kijasusi wa utawala wa Kizayuni wa Israel. Vile vile amevujisha taarifa nyingi zinazohusiana na umeme wa nyuklia wa Iran kwa mashirika ya kijasusi ya madola tofauti ya kigeni.
Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Mahakama ya Mapinduzi ya Tehran pia amesema, jasusi huyo alivujisha taarifa hizo za kijasusi za mradi wa Iran wa kuzalisha umeme kwa kutumia nishati ya nyuklia baada ya kupewa Euro laki moja na 40 elfu. Amesisitiza kwa mara nyingine kuwa, jasusi huyo amepewa adhabu ya kifungo cha miaka 10 jela.