Rouhani: Iran itakabiliana ipasavyo na Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i40023-rouhani_iran_itakabiliana_ipasavyo_na_marekani
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, iwapo Washington itaiwekea mashinikizo Tehran, Jamhuri ya Kiislamu itakabiliana ipasavyo na Marekani.
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Feb 06, 2018 23:53 UTC
  • Rouhani: Iran itakabiliana ipasavyo na Marekani

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, iwapo Washington itaiwekea mashinikizo Tehran, Jamhuri ya Kiislamu itakabiliana ipasavyo na Marekani.

Rais Hassan Rouhani aliyasema hayo jioni ya jana katika mkutano na waandishi wa habari mjini Tehran. Ameashiria matamshi ya Rais Donald Trump wa Marekani kuhusu kurejeshwa vikwazo dhidi ya Iran na kusema: Marekani daima imekuwa ikifanya njama za kulisababishia matatizo taifa na serikali ya Iran kupitia njia ya vikwazo na mashinikizo lakini uhusiano wa Iran na nchi nyingine duniani unaboreka zaidi. 

Kuhusu hatua itakayochukuliwa na Iran iwapo Marekani itatupilia mbali makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, Rais Rouhani amesema kuwa: Iran haitakuwa ya kwanza kukiuka makubaliano hayo lakini Tehran imebuni taratibu za kukabiliana na hali hiyo. Amesema makubaliano ya JCPOA ni mkataba wa kimataifa uliopasishwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na makubaliano hayo hayatapunguzwa wala kuongezewa lolote.

Dakta Hassan Rouhani

Kuhusu sisitizo la nchi za Magharibi la kufanyika mazungumzo juu ya makubaliano ya nyuklia ya JCPOA na uwezo wa makombora ya Iran, Dakta Rouhani amesema: Tutatatayarisha chochote tunachokihitajia katika masuala ya ulinzi na kujihami lakini wakati huo huo Tehran inakutambua kutengeneza makombora kwa ajili ya kuua watu wasio na hatia katika nchi nyingine kuwa ni kinyume na maadili na mafundisho ya dini. 

Vilevile amelaani kuwepo kwa majeshi ya Marekani nchini Syria na kusema: Wamarekani wanataka kuigawa nchi hiyo.

Rais Rouhani akizungumza na waandishi wa habari, Tehran

Kuhusu mwenendo wa baadhi ya nchi za Kiarabu kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema: Baada ya kupita muda watawala wa Riyadh huko Saudi Arabia wataelewa kwamba, wamechagua njia isiyo sahihi ambayo haiwezi kuwafikisha popote. Amesisitiza kuwa utawala wa Kizayuni wa Israel ni adui wa mataifa yote ya Mashariki ya Kati na adui wa Waislamu wote.