Wall Street Journal: Iran imepuuza wito wa mazungumzo wa Marekani
Gazeti la Wall Street Journal la Marekani limeandika kuwa serikali ya Washington imejaribu kufungua njia za kufanya mazungumzo na Tehran lakini Iran imepuuza wito huo.
Wall Street Journal limeandika kuwa, serikali ya Donald Trump iliamua kushika njia hiyo baada ya kufeli siasa zake za mashinikizo na vikwazo dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Ripoti ya Wall Street Journal imesema kuwa, mwezi Disemba mwaka jana White House ilituma ujumbe kwa Tehran kwa kisingizio cha suala la kuachiwa huru wafungwa wa pande hizo mbili ikitaka kuwepo mawasiliano ya moja kwa moja baina ya pande hizo mbili. Limeongeza kuwa hata hivyo baada ya kupita miezi miwili sasa tangu ombi hilo lilipotolewa na kutolewa mapendekezo mengine matatu mtawalia ya Washington juu ya kuanzishwa mazungumzo, Iran imepuuza wito huo.
Awali Naibu Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani, Steve Goldstine alieleza hamu ya Washington ya kufanya mazungumzo na viongozi wa serikali ya Tehran.
Ni vyema kuashiria hapa kuwa, tangu baada ya Donald Trump kushika madaraka nchini Marekani, Washington imekuwa ikizidisha uhasama na mashinikizo dhidi ya Iran ikiwa ni pamoja na kutaka kuvuruga utekelezaji wa makubaliano ya nyuklia ya JCPOA kati ya Iran na kundi la 5+1.