Qassemi: Al Jubeir anabwabwaja, anataka kuzungumza kwa niaba ya Wairaqi
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i40411-qassemi_al_jubeir_anabwabwaja_anataka_kuzungumza_kwa_niaba_ya_wairaqi
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amejibu madai yaliyotolewa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia katika kikao cha kuijenga upya Iraq dhidi ya Iran na kusema: Adel al-Jubeir amesahau kwamba hawezi kuzungumza kwa niaba ya serikali ya Iraq na wananchi wa nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 15, 2018 12:49 UTC
  • Qassemi: Al Jubeir anabwabwaja, anataka kuzungumza kwa niaba ya Wairaqi

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amejibu madai yaliyotolewa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia katika kikao cha kuijenga upya Iraq dhidi ya Iran na kusema: Adel al-Jubeir amesahau kwamba hawezi kuzungumza kwa niaba ya serikali ya Iraq na wananchi wa nchi hiyo.

Bahram Qassemi amesema kuwa, serikali na taifa la Iraq na nchi nyingine zinazoona mbali na kutambua uhakika wa mambo, daima zinajua nafasi na mchango mkubwa wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika kuimarisha amani na utulivu, kupambana na ugaidi wa makundi ya kifakfiri katika Mashariki ya Kati na huko Iraq na kuimarisha amani nchini humo na kwamba, madai yaliyotolewa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia, Adel al-Jubeir hayana maana kiasi kwamba hayastahiki hata kujibiwa. 

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema inasikitisha kuona kwamba, Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudia amekuwa na ada ya kubwabwaja na kutoa maneno bila kutafakari na yasiyo ya kuwajibika. 

Al Jubeir

Katika matamshi yake kwenye mkutano wa kimataifa wa kiujenga upya Iraq unaofanyika nchini Kuwait Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia, Adel al-Jubeir ameendelea kutoa madai yasiyo na msingi dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kudai kuwa uingiliaji wa Iran katika masuala ya ndani ya Iraq unahatarisha usalama na utulivu wa nchi hiyo.

Vilevile amedai kuwa, Tehran imekuwa na nafasi hasi na haribifu huko Iraq. 

Madai hayo ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia yametolewa katika hali ambayo maafisa wa serikali ya Iraq wamekuwa wakisifu na kupongeza nafasi na mchango wa Jamhuri ya Kiislamu katika kuwasaidia Wairaqi na katika kupambana na kuliangamiza kundi la kigaidi la Daesh.