Rais Rouhani: Uhusiano wa Iran na India hauna madhara kwa nchi yoyote
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i40505-rais_rouhani_uhusiano_wa_iran_na_india_hauna_madhara_kwa_nchi_yoyote
Rais Hassan Rouhani amesema uhusiano wa Iran na India hauna madhara kwa nchi yoyote na kubainisha kuwa kuna fursa nyingi za kustawisha na kuimarisha uhusiano wa pande mbili ambazo zinapasa kutumiwa zaidi kwa ajili ya manufaa na mustakabali bora wa mataifa hayo mawili na eneo kwa ujumla.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 17, 2018 14:22 UTC
  • Rais Rouhani: Uhusiano wa Iran na India hauna madhara kwa nchi yoyote

Rais Hassan Rouhani amesema uhusiano wa Iran na India hauna madhara kwa nchi yoyote na kubainisha kuwa kuna fursa nyingi za kustawisha na kuimarisha uhusiano wa pande mbili ambazo zinapasa kutumiwa zaidi kwa ajili ya manufaa na mustakabali bora wa mataifa hayo mawili na eneo kwa ujumla.

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameyasema hayo leo mjini New Delhi katika mazungumzo na Waziri Mkuu wa India Narendra Modi, ambapo amezitaja sekta zinazohusiana na nishati na usafiri kuwa ni fursa mbili muhimu kwa ajili ya ushirikiano wa kistratijia wa nchi mbili na kuongeza kwamba: Bandari ya Chabahar, ambayo ni daraja linalounganisha India na Afghanistan, Asia ya Kati na Ulaya Mashariki, inaweza kuuimarisha zaidi uhusiano wa kihistoria wa Iran, India na eneo.

Dakta Rouhani amesisitiza pia kwamba: Iran inaweza kukidhi mahitaji ya nishati inayohitajiwa na India kupitia mikataba ya kistratijia ya muda mrefu.

Katika mazungumzo yake hayo na Waziri Mkuu wa India, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameutaja ugaidi kuwa ni tatizo sugu kwa dunia na kubainisha kwamba inapasa kupambana na chimbuko la ugaidi, ambalo zaidi ni la kifikra na kiutamaduni na linalotokana na uenezaji fikra za misimamo mikali ya kufurutu mpaka inayoshajiisha ukatili, na kuongeza kuwa Iran iko tayari kushirikiana kiutamaduni na nchi rafiki ikiwemo India katika suala hilo.

Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Iran na India baada ya kusaini hati ya maelewano

Kwa upande wake, Waziri Mkuu wa India Narendra Modi amesema nchi yake iko tayari kuwa na ushirikiano wa muda mrefu na Iran katika nyanja zote kulingana na ridhaa ya nchi mbili na kuongeza kwamba mashirika ya India yako tayari kuwekeza mitaji yao katika nyanja za ushirikiano wa pamoja ikiwemo sekta ya mafuta na gesi.

Wakati huohuo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na India zimesaini hati 15 za maelewano kwa ajili ya ushirikiano katika sekta mbalimbali zikiwemo za biashara, kilimo, afya, posta, ubadilishanaji wa wahalifu pamoja na masuala ya viza.

Hati hizo zimetiwa saini leo na mawaziri na maafisa wa ngazi za juu wa nchi mbili kwa kuhudhuriwa na Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Waziri Mkuu wa India.

Rais Rouhani na ujumbe wa ngazi za juu alioufuatana nao aliwasili nchini India siku ya Alkhamisi katika safari ya siku tatu iliyoanzia katika mji wa Haidarabad, kusini mwa nchi hiyo.../