IAEA: Iran imeheshimu makubaliano ya nyuklia ya JCPOA
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i40741-iaea_iran_imeheshimu_makubaliano_ya_nyuklia_ya_jcpoa
Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) umethibitisha tena kwamba, shughuli za miradi ya kuzalisha nishati ya nyuklia nchini Iran zinafanyika kwa mujibu wa makubaliano ya nyuklia ya JCPOA.
(last modified 2026-08-17T09:53:57+00:00 )
Feb 22, 2018 23:48 UTC
  • IAEA: Iran imeheshimu makubaliano ya nyuklia ya JCPOA

Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) umethibitisha tena kwamba, shughuli za miradi ya kuzalisha nishati ya nyuklia nchini Iran zinafanyika kwa mujibu wa makubaliano ya nyuklia ya JCPOA.

Mkurugenzi Mkuu wa wakala huo, Yukia Amano amesema katika ripoti yake ilkiyotolewa jana Alkhamisi kwamba Iran imeheshimu na kutekeleza makubaliano ya nyuklia ya JCPOA na kuongeza kuwa, Tehran imeueleza wakala huo uamuzi wake wa kutaka kujenga taasisi nyingine ya nyuklia ya baharini.

Ripoti mpya ya Amano kuhusu hali ya miradi ya kuzalisha nishati ya nyuklia nchini Iran imesisitiza kuwa, Iran imeheshimu kiwango kilichoainishwa cha maji mazito na urani iliyorutubishwa. Ripoti hiyo pia imethibitisha kuwa, Iran imeuruhusu Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki kutumia njia za usimamizi zilizopasishwa katika makubaliano ya JCPOA. 

Mwakilishi wa kudumu wa Iran katika Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki, Reza Najafi amesema baada ya kutolewa ripoti hiyo ya 10 ya wakala huo kwamba, imethibitisha tena kuwa, miradi ya kuzalisha nishati ya nyuklia hapa nchini inafanyika kwa mujibu wa makubaliano ya JCPOA. 

Reza Najafi

Makubaliano ya nyuklia kati ya Iran na nchi sita za Russia, Ufaransa, Uingereza, China, Marekani na Ujerumani yalianza kutekelezwa Januari mwaka 2016.