Mar 01, 2018 15:30 UTC
  • Iran yazilaumu vikali nchi zinazomiliki silaha za nyuklia

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amezilaumu vikali nchi zinazomiliki silaha za nyuklia kwa kutoheshimu ahadi zao kwa mujibu wa kifungu cha 6 cha Mkataba wa Kuzuia Uzalishaji, Uenezaji na Utumiaji wa Silaha za Nyuklia na kusema kuwa nchi hizo ndizo zinazokwamisha ufanikishaji wa vipengee vya mkabata huo.

Gholam Hossein Dehghani, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran katika masuala ya sheria na kimataifa amesema hayo kwenye mkutano wa ngazi za juu wa kuangamiza silaha wa mjini Geneva Uswisi na kuongeza kuwa, si tu hadi sasa hakuna maendeleo yoyote yaliyopatikana katika juhudi za kuangamiza silaha za nyuklia duniani lakini pia nchi zinazomiliki silaha hizo hata zimeongeza kasi ya kumiliki silaha za kisasa kabisa na kuwekeza katika kuimarisha na kuzifanya za kisasa zilaha za nyuklia kwa kuzalisha vichwa vipya na vyenye uwezo mkubwa zaidi wa kuangamiza sehemu zinapotumika.

Mripuko wa nyuklia. Kwa mtazamo wa Uislamu silaha hizi ni haramu kutokana na kuangamiza hata viumbe visivyo na hatria wakati zinapotumiwa

 

Amesema, Marekani imewekeza dola trilioni moja na bilioni 250 kwa ajili ya kubadilishwa silaha zake za nyuklia kuwa za kisasa kabisa katika kipindi cha miaka 30 ijayo na jambo hilo limezusha wasiwasi mkubwa duniani.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameongeza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inapinga vikali kumiliki silaha za nyuklia kutokana na itikadi zake za kidini hivyo si ufakhari kwa Tehran kuwa na silaha za nyuklia bali ni haramu kuwa nazo kwa mujibu wa fatwa ya Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu.

Amesisitiza kuwa, Iran ni muungaji mkono mkuu na wa kudumu wa jitihada za kuangamiza silaha za nyuklia duniani na kwamba kuangamizwa silaha hizo na silaha zote za maangamizi ya umati kuna manufaa makubwa kwa Iran kwani siasa za kiulinzi za Iran zimesimama juu ya misingi ya kimantiki, kisheria na itikadi zake za kidini (ambazo zinasisitiza kuwa, kuua mtu mmoja ni sawa na kuua watu wote).

Tags