Qassemi: Saudia ni chanzo kikuu cha ugaidi duniani
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mapema Jumamosi amejibu tuhuma za hivi karibuni za Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudia na kusema,"Saudi Arabia ndio chanzo kikuu cha ugaidi, ukosefu wa usalama na misimamo mikali katika eneo na dunia nzima."
Adel al Jubeir , Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia, siku ya Alhamisi akizungumza katika Taasisi ya Utafiti ya Brookings nchini Marekani aliituhumu Iran kuwa inaunga mkono ugaidi na kuendelea kudai kuwa eti Iran ni tatizo kwa eneo. Hii ni katika hali ambayo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni mhimili na kati ya nguzo kuu za vita dhidi ya ugaidi Asia Magharibi.
Kufuatia maombi rasmi ya serikali za Iraq na Syria, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetuma washauri wa kijeshi katika nchi hizo ili kuzisaidia katika kupambana na magaidi na jambo hilo halikuwafurahisha hata kidogo wakuu wa Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel pamoja na kibaraka wao, Saudi Arabia.
Akihutubu katika taasisi hiyo ya Brookings, Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudia pasina kuashiria namna nchi yake inavyotekeleza jinai za kivita Yemen, amesema njia pekee ya kutatua mgogoro wa nchi hiyo ni kufuata mchakato wa kisiasa.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema al Juberi anazungumza kuhusu utatuzi wa kisiasa wa mgogoro wa Yemen katika hali ambayo kwa miaka mitatu sasa wakuu wa Riyadh wamekuwa wakiweka vizingiti katika jitihada zote za kuutatua mgogoro huo kisiasa.