Waziri wa Ulinzi wa Uingereza acheza ngoma ya Trump
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i42572-waziri_wa_ulinzi_wa_uingereza_acheza_ngoma_ya_trump
Waziri wa Ulinzi wa Uingereza amedai kuwa, kuwepo kwa makundi yanayopigana kwa niaba ya Iran katika nchi za Iraq, Syria na Yemen na eti sera za kupenda jaha ya atomiki za Tehran ni mambo yanayotambuliwa na watu wote!
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 03, 2018 01:59 UTC
  • Waziri wa Ulinzi wa Uingereza acheza ngoma ya Trump

Waziri wa Ulinzi wa Uingereza amedai kuwa, kuwepo kwa makundi yanayopigana kwa niaba ya Iran katika nchi za Iraq, Syria na Yemen na eti sera za kupenda jaha ya atomiki za Tehran ni mambo yanayotambuliwa na watu wote!

Gavin Williamson ametoa madai hayo yasiyo na msingi na kucheza dansi na ngoma inayoendelea kupigwa na Marekani hususan kiongozi wa nchi hiyo, Donald Trump licha ya madai hayo kukanushwa mara kwa mara na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Kabla ya hapo pia Mrithi wa Kiti cha Ufalme wa Saudi Arabia aliyeko safarini nchini Marekani, Muhammad bin Salman alitaka kumfurahisha bwana wake, yaani Donald Trump kwa kudai kuwa, makubaliano ya nyuklia ya Iran na nchi za kundi la 5+1 hayaizuia Jamhuri ya Kiislamu kutengeneza silaha za nyuklia na kwamba kuna haja ya kufanyiwa mabadiliko na kutengeneza makubaliano mengine mbadala.

Trump na Bin Salman

Kwa muda sasa Rais wa Marekani amekuwa akifanya jitihada za kuiondoa nchi hiyo katika makubakliano ya nyuklia ya JCPOA kwa kutumia visingizio mbalimbali. Trump anadai kuwa, njia pekee ya kubakia Marekani katika makubaliano hayo ni kufanyiwa mabadiliko. Miongoni mwa mambo yanayosisitizwa sana katika propaganda za Marekani na baadhi ya nchi za Ulaya hususan Ufaransa na Uingereza na kibaraka wao Saudi Arabia, ni kuingizwa kadhia ya makombora ya Iran katika mkataba wa nyuklia wa JCPOA. Nchi hizo zimekuwa zikifanya propaganda kubwa za kuchafua zaidi jina la Jamhuri ya Kiislamu ili kuvuruga mlingano wa Mashariki ya Kati.

Ukweli ni kwamba, nafasi na mchango chanya wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran umevuruga mahesabu ya kisiasa ya madola makubwa na vibaraka wao katika eneo la Mashariki ya Kati hususan eneo la Asia Magharibi. Iran imefanikiwa kuzima njama na sera za kijuba za baadhi nchi za nje ya eneo hili na kwa sababu hiyo zimeamua kubuni tuhuma zisizo na msingi dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu.

Mtaalamu wa masuala ya Mashariki ya Kati wa Lebanon, Ghalib Qindiil anasema kuhusu nafasi ya Iran katika eneo hilo kwamba: Iran imeweza kuwa na mchango mkubwa na kuuhami kwa nguvu zote mrengo na kambi ya mapambano dhidi ya Wazayuni na mabeberu katika eneo la Mashariki ya Kati, na misaada ya kiuchumi, kijeshi na ya kitaalamu ya Jamhuri ya Kiislamu imekuwa na nafasi muhimu sana katika ushindi uliopatikana dhidi ya makundi ya kigaidi katika eneo hilo."

Makombora ya Iran, jinamizi la mabeberu

 

Vilevile afisa wa Harakati ya Wananchi ya Ukombozi wa Palestina, Saleh Abu Majid anasema: "Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imevuruga mahesabu ya maadui wake katika medani za kisiasa na kijeshi katika eneo la Mashariki ya Kati kutokana na nguvu yake kubwa."

Waziri wa Ulinzi wa Uingereza amedai Iran inaendeleza sera za kutafuta jaha ya nyuklia na kupuuza uhakika kwamba, kwanza kutokana na sera zake za kiulinzi, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haina nia ya kumiliki silaha za nyuklia. Katika uwanja huo pia fatwa iliyotolewa na Kiongozi Mkuu wa Iran akiharamisha silaha hizo za nyuklia ni msingi imara na ushahidi wa wazi wa ukweli huo. Pili ni kwamba, tangu uliopanza kutekelezwa mkataba wa nyuklia wa JCPOA Januari 2016 Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) umetoa ripoti 10 mtawalia ukisisitiza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeheshimu na kutekeleza majukumu yake yote yaliyoainishwa ndani ya makubaliano hayo na kwamba miradi yake ya nyuklia inafanyika kwa malengo ya amani.

Mkurugenzi wa wakala wa IAEA

Kwa msingi huo inabainika kuwa, chokochoko za maafisa wa nchi za Ulaya na Marekani na vibaraka wao wa kikanda hususan Saudi Arabia kuhusu miradi ya nyuklia na uwezo wa makombora ya Iran zinafanyika kwa lengo la pamoja nalo ni kuibana Iran na hatimaye nchi hizo kushika usukani wa kuendesha msuala ya Mashariki ya Kati kwa mujibu wa sera na siasa zao.