Mtazamo wa Kiongozi Muadhamu: Kushadidisha Mapambano na Israel; Tiba Pekee ya Palestina
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika kujibu barua ya hivi karibuni ya Ismail Hania Mkuu wa Idara ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina, Hamas, ametilia mkazo msimamo wa daima wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wa kuiunga mkono kikamilifu Palestina na wapigana jihadi wake na kusema kuwa, tiba ya kadhia ya Palestina ni kuimarishwa mrengo wa mapambano na muqawama.
Ayatullah Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amebainisha zaidi kuwa, hapana shaka kwamba, "muqawama na mapambano ndiyo njia pekee ya kukomboa Palestina inayodhulumiwa na ndiyo dawa pekee ya kuponya majeraha ya mwili wa taifa hilo shujaa na lenye fahari. Ameongeza kuwa, harakati ya kuelekea upande wa kufanya mazungumzo na utawala laghai, mrongo wa ghasibu ni kosa kubwa lisilosameheka ambalo litachelewesha ushindi wa taifa la Palestina, na harakati hiyo haitakuwa na matokeo mengine isipokuwa hasara kwa taifa hilo linalodhulumiwa."
Hivi Kairbuni Mkuu wa Idara ya Siasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina, Hamas, Ismail Hania alimuandikia barua Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, na kushukuru kwa dhatia uungaji mkono wa taifa la Iran na miongozo ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa harakati ya mapambano ya Wapalestina.
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ndiyo nchi pekee duniani ambayo inaunga mkono kwa dhati na kutetea malengo ya taifa linalodhulumiwa la Palestina.
Kuunga mkono mataifa yanayodhulumiwa ili yaweze kupata haki zao ni moja ya misingi mikuu ya sera za kigeni za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na uungaji mkono wa pande zote kwa taifa la Palestina ni nembo ya sera hizi za kimsingi.
Baada ya kusambaratika utawala wa Kipahlavi wa Iran mwaka 1979, utawala ambao ulikuwa ukipata himaya ya utawala wa Kizayuni wa Israel, ubalozi wa utawala huo bandia hapa mcjhini Tehran ulifungwa mara moja na mahala pake kuchukuliwa na ubalozi wa Palestina kufuatia ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu. Mbali na hayo, kwa ubunifu wa Imam Khomeini MA, muasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Ijumaa ya mwisho ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, ilitangazwa kuwa Siku ya Kimataifa ya Quds, kwa lengo la kuunga mkono malengo matukufu ya taifa la Palestina.
Sera za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran zimepelekea kadhia ya Palestina iondoke katika duara la kuwa kadhia ya nchi za Kiarabu tu na kubadilishwa kuwa kadhia ya Kislamu na kimataifa. Leo waliowengi duniani wanahisi namna taifa la Palestina linavyodhulumiwa.
Iran mbali na uungaji mkono wake wa kifedha na kimaanawi kwa harakati za mapambano ya ukombozi wa Palestina, pia katika uga wa kisiasa imekuwa ikifanya jitihada kubwa kutatua kaadhia ya Palestina. Iran imewasilisha mpango wa kisiasa wa kutatua kadhia ya Palestina unaojumuisha kushiriki Wapalestina wote, wakiwemo walio nje ya ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu, katika kura ya maamuzi ili kuamua mustakabali wao.
Iran inaitazama kadhia ya kuundwa taifa la Palestina kwa mtazamo wa kutoka 'Mto Hadi Baharini', yaani kutoka Mto Jordan hadi Bahari ya Mediterania. Mpango huu umepingwa vikali na utawala wa Kizayuni wa Israel, Wamarekani na waitifaki wao.
Hivi sasa kuna baadhi ya madola ya Kiarabu ambayo yamehusika katika uhaini wa kuvuruga utatuzi wa kisiasa wa kadhia ya Palestina na yanajaribu kulazimisha kuwepo uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni kwa lengo la kufuta 'Mapamabano au Muqawama na Intifadha' ambayo ni mkondo uliojaa fahari wa vijana wa Palestina katika historia ya miaka 70 ya mapambano yao dhidi ya utawala ghasibu wa Israel.
"Intifadha ya Kwanza, Intifadah ya Pili na Hivi sasa Intifadha ya Quds" imebadilika kuwa kiashiria cha uwezo wa kufikia malengo matukufu ya Wapalestina katika mhimili wa 'Kurejea Wakimbizi Wapalestina' katika ardhi zao za jadi.
Kuendelea mapambano ya silaha katika kukabiliana na utawala ghasibu na wa kibaguzi wa Israel ni jambo ambalo limeleta ushindi katika malengo matukufu ya Wapalestina. Kufeli mpango wa kuweka vizuizi vya kiusalama katika Msikiti wa Al Aqsa mwaka uliopita wa 2017 hadi sasa, na kushiriki kwa wingi Wapalestina katika maandamano makubwa ya 'Haki ya Kurejea" ni kilele cha kushadidi mapambano mbele ya kujitakia makuu utawala ghasibu wa Israel na waitifaki wake.
Kujitokeza kwa wingi vijana wanamapambano wa Kipalestina katika maandamano ya 'Haki ya Kurejea' ni dhihirisho la 'uwezo wa wananchi katika Intifadha' na ni indhari kwa wakuu wa utawala wa Kizayuni, Marekani na baadhi ya watawala wa Kiarabu kuwa jaribio lolote la kutekeleza kile wanachodai kuwa ni 'muafaka wa karne', yaani kuwanyima Wapalestina haki ya kurejea katika ardhi zao za jadi' ni muafaka ambao utakabiliwa na jibu kali la wanamapambano.
Ushirikiano wa pande tatu, yaani utawala wa Kizayuni wa Israel, Marekani na Saudi Arabia katika kufuta haki na malengo matukufu ya Wapalestina kwa ajili ya kuuletea usalama utawala unaozidi kudhoofika wa Kizayuni ni ndoto isiyoweza kufikiwa. Mpango wa maelewano na utawala wa Kizayuni umeshika kasi wakati huu wa utawala wa Rais Donald Trump wa Marekani na sasa unaungwa mkono na utawala wa Saudia kupitia misamiati mipya.
Ni katika mazingira kama hayo ndio kukawa na udharura wa "kushadidisha na kuimarisha mhimili wa muqawama katika ulimwengu wa Kiislamu na Palestina" ili kusambaratisha njama hizo.