Ayatullah Khatami: Kuitambua rasmi Israel ni doa baya kwa Saudi Arabia
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i42732-ayatullah_khatami_kuitambua_rasmi_israel_ni_doa_baya_kwa_saudi_arabia
Khatibu wa Swala ya Ijumaa iliyoswaliwa leo hapa mjini Tehran amesema kuwa, hatua ya Saudi Arabia ya kuutambua rasmi utawala haramu wa Israel kumeitia doa baya utawala wa Aal Saud.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 06, 2018 09:47 UTC
  • Ayatullah Khatami: Kuitambua rasmi Israel ni doa baya kwa Saudi Arabia

Khatibu wa Swala ya Ijumaa iliyoswaliwa leo hapa mjini Tehran amesema kuwa, hatua ya Saudi Arabia ya kuutambua rasmi utawala haramu wa Israel kumeitia doa baya utawala wa Aal Saud.

Ayatullah Ahmad Khatami amesema hayo leo mbele ya hadhara ya waumini waliohudhuria ibada ya Swala ya Ijumaa mjini Tehran na kubainisha kwamba, hujuma ya kijeshi ya utawala vamizi wa Israel dhidi ya Lebanon na Gaza katika miaka ya hivi karibuni ilifanyika kwa misaada ya kifedha na ushajiishaji wa Saudi Arabia.

Khatibu wa Swala ya Ijumaa mjini Tehran amebainisha kwamba, utawala wa Saudia unapaswa kushtakiwa katika mahakama ya Kiislamu kutokana na kuyaunga kwake mkono makundi ya kigaidi na kitakfiri na kuwa na nafasi kubwa katika kumwaga damu zisizo na hatia ulimwenguni zikiwemo damu za wananchi wa Yemen.

Mfalme Salman bin Abdul Aziz, mfalme wa Saudi Arabia

Ayatullah Khatami amesema pia kuwa, Saudi Arabia ni mshirika wa uhalifu wa utawala haramu wa Israel na kuongeza kuwa, utawala wa Riyadh ulitoa mabilioni ya dola kwa ajili ya kuingilia uchaguzi wa Iraq na Lebanon, lakini hivi sasa kuna kila ishara za kutetereka utawala huo wa Aal Saud.

Khatibu wa Swala ya Ijumaa  mjini Tehran ameashiria jinai za Israel na mauaji yake dhidi ya Wapalestina katika maandamano ya "Haki ya Kurejea" na kusema kwamba, uwepo na asili ya utawala huo ghasibu ni kufyonza damu na hakuna jibu mwafaka kwa utawala huo isipokuwa mpambano.

Ayyatullah Khatami amekosoa vikali kimya cha nchi za Kiislamu kwa jinai za Israel na kusema kuwa, matamshi ya mamufti wa Saudia na fatuwa zao za kuharamisha maandamano ya kuiunga mkono Gaza na ambazo zimepokolewa kwa shangwe na Wazayuni ni usaliti na vitendo vilivyo dhidi ya Uislamu.