Feb 02, 2024 13:58 UTC
  • Khatibu wa Sala ya Ijumaa mjini Tehran: Iran ni nchi huru zaidi duniani

Khatibu wa Sala ya Ijumaa iliyosaliwa leo mjini Tehran ameitaja Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuwa nchi huru zaidi duniani.

Ayatullah Seyyed Ahmad Khatami, Khatibu wa muda wa Sala ya Ijumaa mjini Tehran katika khutba zake za Sala ya Ijumaa amezitaja tawala za kifalme za Qajar na Pahlavi, ambazo ziliwahi kutawala Iran miongo ya nyuma kuwa ni vibaraka wa ajinabi na akasema: "Kufuatia ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Iran ilipata uhuru na tunajivunia kwamba leo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni nchi huru zaidi duniani. 

Ayatullah Khatami, ameashiria kuwadia siku za maadhimisho ya ushindi wa  Mapinduzi ya Kiislamu na kuongeza kuwa, ushiriki mkubwa katika matembezi ya tarehe 22 Bahman sawa na 11 Februari  utakuwa ni kushukuru neema zitokanazo na ushindi wa mapinduzi hayo. Halikadhalika amesema kushiriki katika uchaguzi wa tarehe 11 Esfand sawa na Machi 1 wa Majlisi ya Ushauri wa Kiislamu (Bunge la Iran) na Baraza la Wanazuoni Wataalamu wanaomchagua Kiongozi Muadhamu pia ni kutoa shukrani kwa ajili ya neema na baraka za utawala wa Kiislamu, uhuru na kujitegemea nchi.

Hali katika Ukanda wa Gaza wakati huu wa vita vya mauaji ya kimbari vya Israel dhidi ya Wapalestina eneo hilo

Khatibu wa muda wa Sala ya Ijumaa ya wiki hii mjini Tehran sambamba na kulaani kuendelea mashambulizi ya utawala wa Kizayuni wa Israel katika Ukanda wa Ghaza amesisitiza kuwa: "Ushindi wa mwisho hatimaye utakuwa ni wa taifa la Palestina".

Ayatullah Khatami ameashiria tangazo la Qatar kuhusiana na hatua katika mazungumzo ya usitishaji vita huko Gaza  na kuongeza  kuwa: Masharti mawili ambayo Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) imeyaweka katika usitishaji vita,  yaani kusitishwa kikamilifu kwa mashambulizi yote ya  utawala wa Israel na kubadilishana wafungwa wote ni ya kimantiki lakini wakati huo huo Wapalestina wanapaswa kuwa macho.

Tangu tarehe 7 Oktoba 2023, zaidi ya Wapalestina 27,000, wengi wakiwa ni wanawake na watoto wameuawa shahidi na wengine zaidi ya 66,000 wamejeruhiwa katika mashambulizi ya jeshi la utawala huo kwenye maeneo mbalimbali ya Ukanda wa Gaza.

Tags