Jaberi Ansari afanya mazungumzo na mjumbe wa UN katika masuala ya Syria
Mjumbe maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Syria leo amekutana na kufanya mazungumzo hapa mjini Tehran na Hossein Jaberi Ansar msaidizi mkuu wa Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran katika masuala ya siasa.
Pamoja na mambo mengine wawili hao wamejadili matukio ya hivi karibuni nchini Syria.
Hossein Jaberi Ansari, msaidizi mkuu wa Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran katika masuala ya siasa amewaambia waandishi wa habari baada ya mazungumzo yake na Staffan de Mistura kwamba, utatuzi wa mgogoro wa Syria ni kuikubali irada na matakwa ya wananchi hao.
Hossein Jaberi Ansari amebainisha kwamba, juhudi za pamoja za washiriki wa mchakato wa mazungumzo ya Astana, Sochi na Geneva zinaweza kuwa na mafanikio pale zitakapoandaa uwanja wa kurahisisha maamuzi ya wananchi wa Syria kwa ajili ya mustakabali wa nchi yao.
Ameongeza kuwa: 'Moja ya malengo ya pamoja sisi sote ni kufanya juhudi kuhakikisha kwamba, ubunifu wote unaofanyika uwe ni kwa ajili ya kulinda mamlaka ya kujitawala ardhi yote ya Syria.'
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ikiwa moja ya nchi zenye taathira kubwa katika Mashariki ya Kati daima imekuwa ikisisitiza juu ya kupatiwa ufumbuzi migogoro yote kupitia mazungumzo na njia za kisiasa ukiwemo mgogoro wa Syria.
Ni kwa kuzingatia ukweli huo ndio maana mazungumzo ya Astana yalianza Januari mwaka jana kwa ubunifu wa Iran na kwa ushirikiano wa Russia na Uturuki lengo likiwa ni kurejesha amani na utulivu nchini Syria.