Iran na Benin kuimarisha uhusiano wao katika uga wa viwanda
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i43516-iran_na_benin_kuimarisha_uhusiano_wao_katika_uga_wa_viwanda
Balozi wa Benin hapa mjini Tehran, Naim Akibo amesema akthari ya nchi za Afrika hazijadiriki uwezo mkubwa wa Iran katika nyuga za viwanda, kilimo na uchumi ambao zingeutumia katika kuimarisha uhusiano na ushirikiano wa pande mbili.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 22, 2018 20:55 UTC
  • Iran na Benin kuimarisha uhusiano wao katika uga wa viwanda

Balozi wa Benin hapa mjini Tehran, Naim Akibo amesema akthari ya nchi za Afrika hazijadiriki uwezo mkubwa wa Iran katika nyuga za viwanda, kilimo na uchumi ambao zingeutumia katika kuimarisha uhusiano na ushirikiano wa pande mbili.

Akibo amesema mataifa ya Afrika hayana ufahamu mkubwa kuhusu uwezo wa kiuchumi wa Iran na ndiposa yamekuwa yaking'ang'ania kufanya biashara na kuimarisha uhusiano na nchi nyingine za bara Asia kama vile China, Korea Kusini na Imarati.

Amesisitiza kuwa, iwapo mashirika ya Iran yataarifisha tajriba na uwezo wao mkubwa kwa nchi za Afrika, basi yatapata soko kubwa katika bara hilo.

Balozi huyo wa Benin amesema nchi yake iko tayari kuimarisha uhusiano wa pande mbili na Iran katika nyuga mbali mbali na hususan kilimo na viwanda.

Rais Rouhani akimpokea Balozi wa Benin mwaka jana

Mwezi Juni mwaka jana, Rais Hassan Rouhani wa Iran alisisitiza kuwa, ni katika sera zilizo madhubuti za nchi hii kuimarisha uhusiano wake na nchi za Afrika. Rais Rouhani aliyasema hayo hapa mjini Tehran wakati akimpokea balozi huyo wa Benin hapa nchini na kuongeza kuwa, Iran na nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika zina fursa nzuri ya kuimarisha uhusiano wa pande mbili katika nyuga mbali mbali.

Dakta Rouhani alisema changamoto zinazoyakabili maeneo hayo mawili ya kistratajia (Afrika na Mashariki ya Kati) hazina suluhu nyingine isipokuwa mazungumzo ya kisiasa.