Ehud Olmert: Israel haina ubavu wa kukabiliana na Iran
Waziri Mkuu wa zamani wa utawala wa Kizayuni wa Israel amesema kuwa, utawala huo hauna ubavu wa kukabiliana na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Ehud Olmert amekiri bayana kwamba, utawala wa Kizayuni wa Israel hauna uwezo wa kuishambulia kijeshi Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Olmert amewatahadharisha viongozi wa sasa wa utawala huo ghasibu na kuwataka wajiepushe na chokochoko ya aina yoyote ile dhidi ya Iran.
Ehud Olmert mwenye umri wa miaka 72 na ambaye aliwahi kuhudumu kama Waziri Mkuu wa Israel mwaka 2006 hadi 2009 amesisitiza kuwa, chokochoko cha aina yoyote ile ya Israel dhidi ya Iran itakuwa hatari kubwa kwa utawala huo vamizi.
Olmert aidha amezungumzia mipango ya Rais Donald Trump wa Marekani na kung'ang'ania Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu kufutwa au kufanyiwa marekebisho makubaliano ya nyuklia ya Iran na kundi la 5+1 na kusema kuwa, anapinga misimamo ya viongozi hao.
Makubaliano ya nyuklia yanayojulikana kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA) yaliyofikiwa kati ya Iran na kundi la 5+1 linalojumuisha nchi za Marekani, Uingereza, Ufaransa, China, Russia pamoja na Ujerumani yalianza kutekelezwa Januari mwaka 2016, hata hivyo serikali ya Washington haijatekeleza majukumu yake ipasavyo kuhusiana na makubaliano hayo. Si hayo tu, bali Marekani imekuwa ikitishia kujitoa katika makubaliano hayo.
Iran nayo kwa upande wake imesisitiza mara kadhaa kwamba, ina machaguo mengi tu mezani kwa ajili ya kukabiliana na kujitoa tarajiwa kwa Marekani katika makubaliano hayo.