Kiongozi: Mguu wa Marekani utakatwa katika eneo
(last modified Mon, 30 Apr 2018 12:57:04 GMT )
Apr 30, 2018 12:57 UTC
  • Kiongozi: Mguu wa Marekani utakatwa katika eneo

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa, "yule ambaye anapaswa kuondoka eneo la Asia Magharibi ni Mmarekani na wala sio Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kama nilivyosema miaka kadhaa iliyopita, zama za utumiaji mabavu zimefika ukingoni."

Ayatullah Sayyed Ali Khamenei ameyasema hayo leo Jumatatu mjini Tehran katika mkesha wa Siku ya Leba (Mei Mosi) wakati alipokutana na maelfu ya wafanyakazi na wajasiriamali mjini Tehran na kuongeza kuwa: "Ghuba ya Uajemi na Asia Magharibi ni nyumba yetu lakini nyinyi ajinabi mnafuatilia malengo khabithi na kuibua fitina."

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria kukosekana usalama na kuenea vita na machafuko Asia Magharibi (Mashariki ya Kati) kutokana na uwepo wa Marekani katika eneo na kusisitiza kuwa: "Ni kwa sababu hii hii ndio mguu wa Wamarekani unapaswa kukatwa katika eneo na waondoke eneo la Asia Magharibi."

Kiongozi Muadhamu amesema moja ya mbinu ambazo Marekani inatumia kukabiliana na mfumo wa kutetea uhuru na wenye kujitegemea wa Jamhuri ya Kiislamu ni kuchochea baadhi ya serikali zenye ufahamu mdogo katika eneo sambamba na kuibua hitilafu na mapigano katika eneo.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu wakati alipokutana na maelfu ya wafanyakazi na wajasiriamali mjini Tehran 30/04/2018

Kiongozi Muadhamu amesema Marekani inajaribu kuichochea Saudia na baadhi ya nchi katika eneo kukabiliana na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran lakini iwapo watakuwa ni wenye akili basi hawatahadaiwa na Marekani.

Ayatullah Khamenei amebaini kuwa, Wamarekani hawataki kugharamika katika kukabiliana na mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu na taifa la Iran hivyo wanataka kuzitwika serikali za eneo gharama hizo. Ameongeza kuwa: "Baadhi ya serikali za eneo zifahamu kuwa, iwapo zitakabiliana na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, bila shaka zitapata pigo na kushindwa."

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aidha amesema njama kuu inayotumiwa hivi sasa katika kukabiliana na mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ni vita vya kiuchumi na kwa msingi huo kusisitiza kuwa njia pekee ya kukabiliana na vita hivyo ni kuunga mkono bidhaa za Kiirani na kutegemea uwezo na vipawa vya ndani ya nchi na kutowategemea ajinabi.

Tags