Rais Rouhani: Iran imeazimia kuimarisha uhusiano na majirani zake ikiwemo Turkmenistan
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kuwa, Tehran imeazimia kwa dhati kuimarisha ushirikiano wake na majirani wote katika nyanja zote ikiwemo Turkmenistan ambayo ni nchi rafiki na ndugu.
Rais Rouhani alisema hayo jana alipokutana na kufanya mazungumzo hapa mjini Tehran na Raşit Meredow, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Turkmenistan na kueleza kuwa, kutekelezwa haraka makubaliano ya pande mbili kutakuwa na manuufaa kwa mataifa hayo mawili.
Rais Hassan Rouhani amesema kuwa, hakuna kikwazo chochote katika njia ya kustawishwa na kuimarishwa zaidi ushirikiano wa Tehran na Ashgabad na kwamba, ni jambo la dharura kwa uhusiano huo kuwepo katika nyuga zote.
Mbali na kutilia mkazo juu ya kustawishwa uhusiano kati ya Iran na Turkmenistan katika nyanja za nishati, umeme, reli na kurahisishwa masuala ya kibiashara, Rais Rouhani ametaka pande mbili hizo zijikite pia katika suala la kupanua ushirikiano wa kielimu, vyuo vikuu na katika uga wa teknolojia ya kisasa.
Kwa upande wake, Raşit Meredow, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Turkmenistan ameashiria katika mazungumzo yake na Rais Rouhani juu ya kuweko mambo ya pamoja ya kiutamaduni na kihistoria baina ya mataifa haya mawili na kusema kuwa, nchi yake imeazimia kwa dhati kabisa kukuza uhusiano na ushirikiano na Jamhuri ya kiislamu ya Iran.