Rais wa Iran ataka dunia isusie Israel, iangalie upya uhusiano na Marekani
Rais Hassan Rouhani wa Iran ametoa wito kwa nchi za Kiislamu na mataifa mengine duniani kukata uhusiano wao kikamilifu na utawala haramu wa Israel na kuangalia upya uhusiano na Marekani kama njia ya kujibu sera hasimu za tawala hizo mbili dhidi ya watu wa Palestina.
Akizungumza katika mkutano wa dharura wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) mjini Istanbul Uturuki Ijumaa, Rais Rouhani amelaani vikali mauaji yaliyofanywa hivi karibuni na utawala wa Israel dhidi ya Wapalestina katika Ukanda wa Ghaza. Aidha amelaani uamuzi wa rais Donald Trump wa Marekani wa kuhamisha ubalozi wa nchi hiyo kutoka Tel Aviv hadi mji wa Quds (Jerusalem) huku akiwasilisha mapendekezo kadhaa kuhuhusu namna ya kuhitimisha sera hizo hasimu.
Rais Rouhani amesema: "Ili kuwasaidia Wapalestina na kukabiliana na uamuzi haribifu wa Trump, tunatoa wito kwa nchi za Kiislamu na mataifa yote yanayopenda uhuru duniani kuangalia upya uhusiano wao wa kisiasa, kiuchumi na kibiashara na Marekani sambamba na kukata uhusiano wote na utawala wa Kizayuni (wa Israel) na kususia bidhaa na mashirika ya Kizayuni."
Rais Rouhani aidha ametaka Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa likutane kujadili hatua iliyo kinyume cha sheria ya Marekani kuhamisha ubalozi wake kutoka Tel Aviv hadi Quds na pia jinai za hivi karibuni za utawala haramu wa Israel huko Ghaza. Rais wa Iran pia ametaka OIC ianzishe mkakati wa kuwafikishia misaada ya kibinadamu Wapalestina na pia kutambuliwa Siku ya Kimataifa ya Quds katika kalenda ya nchi zote za Kiislamu. Rais wa Iran pia ametaka OIC iushinikize utawala haramu wa Israel uangamize silaha zake hatari za nyuklia.
Rais Rouhani amesema utawala wa Kizayuni wa Israel umekuwa ukitekeleza jinai na ukatili dhidi ya Wapalestina kwa miaka sabini sasa na kwamba utawala huo umekiuka sheria na kanunui zote za kimataifa. Rais Rouhani amesema utawala wa Kizayuni umewanyima Wapalestina haki zao za kimsingi na umekuwa ukiwasilisha sera zake za ubaguzi wa rangi na misimamo mikali ya kidini kuwa eti ni demokrasia. Amesema ni jambo la kusikitisha kuwa baadhi ya nchi za Magharibi zimekuwa zikitetea jinai hizo za Israel. Rais Rouhani ametoa wito kwa nchi za Kiislamu kuungana na kuunga mkono harakati za ukombozi wa Palestina.