Rouhani: Njama za Marekani za kuitenga Iran na dunia zimefeli
Rais Hassan Rouhani amesema njama za Marekani za kuitenga Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na dunia zimegonga mwamba licha ya jitihada kubwa za Washington za kufanikisha azma hiyo.
Rais Rouhani amesema watawala wa Washington walidhani kuwa Iran ingefuata nyayo zake za kujiondoa kwenye makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, lakini walipata jibu tofauti na matarajio yao.
Rais wa Iran alisema hayo jana jioni katika mkutano na makundi ya wanawake, wanafunzi na wakuu wa mashirika na kuongeza kuwa, mbali na nchi chache vibaraka wa Marekani, lakini dunia imesimama na Iran licha ya uadui wa Marekani na kwamba jamii ya kimataifa imeipongeza sera thabiti ya kigeni ya Iran.
Amesema hii leo aghalabu ya nchi za Ulaya, Russia na China miongoni mwa nchi nyingine kubwa duniani zinautizama uamuzi wa Donald Trump ya kujiondoa kwenye mapatano hayo ya kimataifa yenye baraka kamili za Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kama ushindi mkubwa kwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Inafaa kukumbusha kwamba Rais Donald Trump wa Marekani alitangaza kuiondoa nchi yake katika makubaliano ya nyuklia ya Iran JCPOA, tarehe 8 mwezi huu sambamba na kutoa tuhuma bandia dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Kadhalika alitoa amri ya kurejeshwa vikwazo vya nyuklia dhidi ya Iran katika kipindi cha kati ya miezi mitatu hadi sita, hatua ambayo imeendelea kukosolewa katika nyuga mbalimbali za kimataifa kutokana na uvunjaji wa wazi wa mikataba ya kimataifa uliofanywa na Marekani.