Rouhani: Marekani haiwezi kuiamulia dunia nzima
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema Marekani haiwezi kuchukua mamuzi kuhusu Iran na nchi zingine huru na zenye kujitegemea duniani.
Kauli hiyo ya Rais Rouhani imekuja baada ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Mike Pompeo kutoa matakwa ambayo eti Washington inataka Iran iyatekeleze katika sera zake za kigeni na za ndani ya nchi.
Akijibu matamshi hayo ya kijuba Jumatatu usiku, Rais Rouhani amesema: "Nchi zote zinataka kuwa huru katika kuchukua maamuzi." Rais wa Iran amesema kuna haja ya nchi kusaidiana kwani utawala wa sasa wa Marekani umerudi nyuma miaka 15 iliyopita na unakariri makosa yale yale ya rais wa zamani wa nchi hiyo George W Bush ambayo aliyafanya mwaka 2003. Rais wa Iran akimuashiria Pompeo ambaye aliwahi kuwa mkuu wa shirika la kijasusi la CIA amesema, 'ni jambo lisilokubalika kwa mtu ambaye alihudumu katika shirika la kijasusi kwa muda mrefu sasa kutoa maamuzi kuhusu Iran na nchi zingine baada ya kuchukua wadhifa wa waziri wa mambo ya nje.' Rais Rouani amehoji zaidi kwa kusema: "Wewe ni nani uchukue maamuzi kuhusu Iran na dunia.?
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Mohammad Javad Zarif naye kupitia ujumbe wa Twitter amemjibu Pompeo kwa kusema Marekani inakariri machaguo mabovu ya huko nyuma na kwamba itapata matokeo yale yale mabaya ambayo iliwahi kuyapata. Amesema udiplomasia wa Marekani ni mbovu na umerejea katika zile tabia za zamani zilizojaa ndoto na sera zilizofeli na zilizoongozwa na maslahi ya kifisadi.