Zarif: Kitendo cha Israel kumuua muuguzi wa Kipalestina ni fedha juu fedheha
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amelaani kitendo cha utawala wa Kizayuni wa Israel cha kumuua shahidi muuguzi wa Kipalestina katika Ukanda wa Ghaza, na kuutaja ukatili huo kama doa jingine kwa utawala huo haramu.
Kupitia ukurasa wake wa Twitter, Mohammad Javad Zarif pia amekosoa vikali hatua ya Marekani kutumia kura yake ya veto kupinga rasimu ya azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linalolaani utumiaji wa nguvu kupita kiasi wa jeshi la Israel dhidi ya Wapalestina.
Dakta Zarif ameandika kwenye ukurasa wake rasmi wa mtandao huo wa kijamii kuwa: "Katika wiki ambayo utawala wa Kizayuni umetuma ujumbe usioeleweka kwa Wairani, mlezi wake Marekani imetumia veto dhidi ya azimio linalolaani utumiaji wa nguvu kupita kiasi dhidi ya waandamanaji ambao hawajajizatiti kwa silaha; na pia ni wiki ambayo walenga shabaha wa utawala huo wamemuua muuguzi wa Kipalestina, aliyekuwa akiwahudumia majeruhi. Fedheha juu ya fedheha!"
Razan al-Najjar, muuguzi wa kujitolea aliyekuwa na umri wa miaka 21 na aliyekuwa akiifanyia kazi Wizara ya Afya ya Ghaza, licha ya kwamba alikuwa amevalia sare rasmi za kazi, lakini aliuawa shahidi kwa kufyatuliwa risasi kifuani, alipokuwa akiwapa matibabu waandamanaji wa Gaza waliojeruhiwa siku ya Ijumaa.
Wakati mauaji hayo ya kinyama yalikuwa yanafanyika siku hiyo ya Ijumaa kwa upande mmoja, Marekani ilikuwa ikitumia kura yake ya turufu kupinga rasimu ya azimio iliyowasilishwa na Kuwait katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, ikitaka kulindwa Wapalestina katika Ukanda wa Ghaza na Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan unaokaliwa kwa mabavu, kwa upande mwingine.
Tokea Machi 30 hadi sasa, utawala haramu wa Israel umewaua shahidi Wapalestina zaidi ya 120 mbali na kujeruhi wengine 13,300, kwa kushiriki katika maandamano ya kutetea haki ya kurejea katika ardhi zao za jadi.