Rouhani: Ushirikiano wa Iran na Russia dhidi ya ugaidi utaendelea
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i45632-rouhani_ushirikiano_wa_iran_na_russia_dhidi_ya_ugaidi_utaendelea
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa kuna umuhimu mkubwa wa kuimarishwa zaidi ushirikiano wa Tehran na Moscow katika masuala ya usalama na ustawi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 09, 2018 12:41 UTC
  • Rouhani: Ushirikiano wa Iran na Russia dhidi ya ugaidi utaendelea

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa kuna umuhimu mkubwa wa kuimarishwa zaidi ushirikiano wa Tehran na Moscow katika masuala ya usalama na ustawi.

Dakta Rouhani ameyasema hayo katika mazungumzo yake ya leo na Rais Vladimir Putin wa Russia na kuongeza kuwa, ushirikiano wa nchi hizo mbili katika masuala ya kupambana na Daesh na makundi mengine ya kigaidi utadumishwa.

Rais Rouhani ambaye anashiriki mkutano wa Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai (SCO) nchini Uchina amesema nchi mbili za Iran na Russia zina uwezo mkubwa kwa ajili ya kupanua zaidi ushirikiano katika masuala ya nishati, ulinzi na usafirishaji na kwamba Tehran inakaribisha uwekezaji wa makampuni na sekta binafsi ya Russia.

Vilevile ameashiria mchango muhimu wa Russia katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA na kusema: Kwa mujibu wa ripoti za Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA), Iran imetekeleza majukumu yake yote, na baada ya Marekani kuondoka kinyume cha sheria katika mapatano hayo, Moscow imekuwa na nafasi muhimu katika kuimarisha makubaliano ya JCPOA na utekelezaji wake. 

Rouhani na Putin

Kwa upande wake Rais Vladimir Putin wa Russia amesisitiza kuwa Moscow itadumisha ushirikiano wake na Tehran katika masuala ya uchumi, nishati na ulinzi na kuongeza kuwa, Moscow pia inaunga mkono suala la Iran kupewa uanachama wa kudumu katika makubaliano ya biashara huru na Urasia na kupewa uanachama kamili katika Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai. 

Putin amesema kuondoka kwa Marekani katika makubaliano ya nyuklia ya Iran ni kinyume cha sheria na hatua ya upande mmoja na kuongeza kuwa, Moscow itaendeleza mazungumzo na pande zote husika kwa ajili ya kulinda makubaliano hayo. 

Rais wa Russia pia amesema kuwa, Moscow itadumisha ushirikiano wake na Iran katika kuimarisha amani na usalama wa Mashariki ya Kati ikiwa ni pamoja na katika kadhia ya Syria.