Kiongozi Muadhamu: Sharti Wapalestina wenyewe waamue hatima ya Palestina
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i45706-kiongozi_muadhamu_sharti_wapalestina_wenyewe_waamue_hatima_ya_palestina
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema hatima ya Palestina inapaswa kuamuliwa na Wapalestina wenyewe, wakiwemo Waislamu, Wakristo na Mayahudi ambao wana asili na waliishi katika ardhi ya jadi ya Palestina.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Jun 11, 2018 07:45 UTC
  • Kiongozi Muadhamu: Sharti Wapalestina wenyewe waamue hatima ya Palestina

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema hatima ya Palestina inapaswa kuamuliwa na Wapalestina wenyewe, wakiwemo Waislamu, Wakristo na Mayahudi ambao wana asili na waliishi katika ardhi ya jadi ya Palestina.

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei aliyasema hayo jana Jumapili, alipokutana na kundi la wahadhiri na wasomi hapa mjini Tehran na kuongeza kuwa: Hii leo, demokrasia ni mfumo wa kisiasa ambao unakubalika na dunia nzima. Tumesema kwamba, kuamua hatima ya nchi ya kihistoria ya Palestina, lazima waulizwe wananchi wenyewe wa Palestina, na pandekezo hili la Jamhuri ya Kiislamu limesajiliwa na Umoja wa Mataifa.

Ayatullah Khamenei amefafanua kuwa, sharti utafiti ufanywe miongoni mwa Wapalestina, ambao wameishi katika ardhi ya Palestina kwa miaka 100 au hata 80, wakiwemo Waislamu, Mayahudi na Wakristo, na kutathmini iwapo wanaishi ndani au nje ya ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu.

Amesema,  "watakachoamua wananchi wa Palestina katika kura hiyo ya maoni sharti kitekelezwa, je hilo ni wazo baya? Je nchi za Ulaya hazipo tayari kufahamu hili?"

Kiongozi Muadhamu katika ukumbi alikohutubia wahadhiri na wasomi

Kadhalika Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria safari ya hivi karibuni ya Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel barani Ulaya iliyokuwa na lengo la kudhalilisha msimamo na nafasi kubwa ya Iran katika eneo na kubainisha kuwa: Huyo dhalimu na muovu (Netanyahu), muuaji wa watoto, anazitembelea nchi nyingine na kujifanya ndiye muhanga na kudai kuwa Iran inataka kuangamiza mamilioni kadhaa ya jamii yake.

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei ameongeza kuwa, Iran ndiyo nchi yenye idadi kubwa ya maadui miongoni mwa serikali za kibeberu duniani, lakini pia kwa upande mwingine ina idadi kubwa ya waungaji mkono katika nchi mbalimbali.