Rouhani: Dunia isimame kidete kukabiliana na ubabe wa Marekani
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema, leo inapasa kuwepo ushirikiano wa watu na nchi zote duniani, washirika wa kibiashara wa Iran, Ulaya, Russia, China na mataifa jirani katika kukabiliana na watawala wa Marekani wanaotumia mabavu na kujifanya wababe.
Rais Hassan Rouhani ameyasema hayo leo asubuhi mjini Tehran katika Baraza la Idul Fitr ambalo limewaleta pamoja viongozi wa ngazi za juu nchini akiwemo Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, wananchi wa matabaka mbali mbali na mabalozi wa nchi za Kiislamu.
Rais Rouhani amesema adui katika hali ya sasa hana uzoefu wala mantiki na kuongeza kuwa: "Uamuzi wa adui ni kwamba si tu asitekeleze ahadi alizotoa kuhusu taifa la Iran bali pia akiuke mapatano na ahadi zote alizotoa kieneo na kimataifa."
Rais Hassan Rouhani ameendelea kusema kuwa ni jambo la kushangaza kuwa dola ambalo mikono yake imejaa damu ya watu wa Iraq, Syria, Yemen na Afghanistan leo linajidai kuwa mtetezi wa amani na linadai kuwa linataka mazungumzo.
Rais wa Iran ameongeza kuwa, waziri mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel, ambao unaua watu wasio na hatia kila siku, anazunguka akieneza hadaa na kujaribu kuichafulia jina Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na watu wake.
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika sehemu nyingine ya hotuba yake amesisitiza ulazima wa kuimarisha mazingira ya kimaanawi, umoja na matumaini kuhusu mustakabali katika taifa la Iran.