Zarif: Wakati wa kuzungumzia vichwa vya nyuklia vya utawala wa Kizayuni umewadia
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema, kuna vichwa visivyopungua 80 vya nyuklia katika Mashariki ya Kati na hakuna hata kimoja kati ya vichwa hivyo vya nyuklia kilichoko ndani ya ardhi ya Iran.
Dakta Zarif ameashiria nukta hiyo katika ukurasa wake wa kijamii wa Twitter na kuongeza kuwa: "Vichwa hivi vinamilikiwa na mshupalia vita anayebweka kiuongo juu ya kile anachodai eti ni "Upenda jaha wa Wairani".
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amefafanua kuwa: "Huu ndio wakati wa kuanza kuzungumzia tishio halisi la eneo na dunia, suala ambalo limecheleweshwa kwa muda mrefu."
Utawala wa Kizayuni wa Israel unaoendesha shughuli zake za nyuklia kwa kificho huku ukiungwa mkono na Marekani hauko tayari kujiunga na Mkataba wa NPT unaopiga marufuku uundaji na uenezaji silaha za nyuklia. Utawala huo wa haramu ambao unazalisha na kurundika silaha za atomiki pamoja na silaha za kemikali katika ardhi ya Palestina unayoikalia kwa mabavu na kuligeuza eneo la Mashariki ya Kati kuwa ghala kubwa la silaha za mauaji ya halaiki ni tishio na hatari kubwa eneo hili na dunia nzima kwa ujumla.../