Ayatullah Khamenei: "Siasa za Kishetani' za Marekani kuhusiana na Palestina katu hazitafanikiwa
Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa, siasa za kishetani za Marekani kuhusiana na Palestina kamwe hazitafanikiwa.
Ayatullah Ali Khamenei amesema hayo leo asubuhi alipokutana na maafisa wa kusimamia ibada ya Hija wa nchini Iran ambapo ameashiria jinsi maadui walivyojizatiti kwa ajili ya kukabiliana na Waislamu hususan kadhia ya Palestina na masuala yanayohusiana na Yemen na kubainisha kwamba, hivi sasa Marekani imezipa siasa zake za kishetani kuhusiana na Palestina jina la 'Muamala wa Karne', lakini wanapaswa kutambua kwamba, kwa fadhila za Mwenyezi Mungu, muamala huo wa karne katu hautafanikiwa kufikia malengo yake na viongozi wa Marekani hawatafanikiwa kuushuhudia kwa macho yao mpango huo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa, kadhia ya Palestina haitasahaulika na Quds utabakia kuwa mji mkuu wa taifa la Palestina.
Ayatullah Khamenei amesisitiza kuwa, taifa la Palestina litasimama imara mbele ya njama za maadui na mataifa ya Kiislamu nayo yataliunga mkono taifa madhulu la Palestina.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran amebainisha wazi kwamba, baadhi ya madola ya Kiislamu ambayo tab'ani hayana imani na Uislamu, yamejitolea kwa ajili ya Wamarekani kutokana na ujinga, ujahili na tamaa za dunia yaliyonayo; hata hivyo kwa tawfiki ya Mwenyezi Mungu, Umma wa Kiislamu na taifa la Palestina watawashinda maadui na wataishuhudia ile siku ambayo mizizi ya utawala bandia wa Israel itakapong'olewa katika ardhi za Palestina.