Sep 04, 2018 13:32 UTC
  • Ayatullah Jannati: Kujiondoa Marekani katika mapatano ya nyuklia ya Iran liwe funzo

Mwenyekiti wa Baraza la Wanazuoni Wataalamu Wanaomchagua Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ahamad Jannati ameashiria Marekani kuvunja ahadi zake na kujiondoa katika mapatano ya nyuklia ya Iran, JCPOA, na kusema hilo linapaswa kuwa funzo kuhusu mazungumzo na Marekani.

Ayatullah Jannati ameyasema hayo leo Jumanne katika ufunguzi wa kikao cha tano cha awamu ya tano ya Baraza la Wanazuoni Wataalamu Wanaomchagua Kiongozi Muadhamu na kuongeza kuwa: "Hakuna maana kufanya mazungumzo na mtu ambaye hafungamani na ahadi zake. Nchi za Ulaya nazo pia hazijatoa dhamana ya kutosha kuhusu kulinda mapatano ya JCPOA."

Ayatullah Jannati ameendelea kusema kuwa, hakuna njia nyingine ya kutatua matatizo ya Iran isipokuwa kuwakabidhi vijana waumini na wanamapinduzi majukumu ya usimamizi. Amesema Kiongozi Muadhamu huwasilisha njia za kutatua matatuzi kwa vyombo husika vya dola na hivyo ni jukumu la vyombo hivi kuwajibika.

Kikao cha tano cha awamu ya tano ya Baraza la Wanazuoni Wataalamu Wanaomchagua Kiongozi Muadhamu

Mwenyekiti wa Baraza la Wanazuoni Wataalamu Wanaomchagua Kiongozi Muadhamu amesisitiza kuhusu ulazima wa kupambana na ufisadi wa kiuchumi na kuongeza kuwa, vyombo vya  mahakama vinapaswa kulipa suala hili umuhimu mkubwa. Aidha amesema kuna ulazima wa kupambana na mafisadi wakubwa ili vita dhidi ya ufisadi viwe na taathira.

Ayatullah Jannati  ameendelea kusema kuwa utatu unaoleta pamoja Saudi Arabia, Marekani na Utawala wa Kizayuni unalenga mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na tishio hilo linapaswa kubadilishwa kuwa fursa kupitia kuimarisha na kutumia vizuri uzalishaji wa ndani ya nchi.

 

Tags