Nchi za dunia zinapaswa kushirikiana na Iran katika kukabiliana na mihadarati
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inasema nchi zote ambazo zinafaidika na jitihada zake za kupambana na mihadarati zinapaswa kuisaidia kiufundi na kifedha.
Hayo yamesemwa na Gholam Hussein Dehqani, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran akiwa mjini Moscow, Russia kuhudhuria Kongamano la Kimataifa la Kukabiliana na Biashara Haramu ya Silaha na Ugaidi wa Kimataifa.
Akizungumza na Yuri Fedotov Mkurugenzi Mtendaji wa Idara ya Kukabiliana na Jinai na Mihadarati katika Umoja wa Mataifa, Dehqani ameongeza kuwa katika miaka ya hivi karibuni idadi kubwa ya maafisa wa usalama wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wameuawa shahidi wakiwa mstari wa mbele kuzuia biashara haramu ya dawa za kulevya.
Aidha amesema Iran imechukua hatua kali katika kukabiliana na biashara ya dawa za kulevya na uhalifu wa kimataifa ulioratibiwa kwani mawili hayo yana uhusiano wa karibu na ugaidi. Ameongeza kuwa leo kote duniani na hasa Asia Magharibi, chanzo kiku cha fedha za magaidi ni biashara ya dawa za kulevya.
Kwa upande wake, Yuri Fedotov, amesema anakubaliana na mtazamo wa Iran kuhusu vita dhidi ya mihadarati na kusema Umoja wa Mataifa utashirikiana na Tehran katika uga huo.
Kongamano la siku mbili la Kimataifa la Kukabiliana na Biashara Haramu ya Silaha na Ugaidi wa Kimataifa lilimalizika jana mjini Moscow na lilijadili njia za kuzuia silaha kuwafikia magaidi.
Hivi karibuni Jenerali Masoud Zahedian, Mkuu wa Kitengo cha Kupambana na Mihadarati katika Jeshi la Polisi la Iran alisema tokea Marekani iivamie kijeshi Afghanistan mwka 2001, uzalishaji wa dawa za kulevya au mihadarati aina ya afiuni umeongezeka mara 22. Idadi kubwa ya wafanya biashara ya mihadarati hujaribu kusafrisha afiuni ya Afghanistan kupitia Iran kutokana na nchi hizi mbili kuwa na mpaka wa pamoja.