Yukiya Amano asisitiza tena kwamba, Iran imetekeleza ahadi zake kuhusu JCPOA
Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) amesisitiza kwa mara nyingine tena kwamba, Iran imekuwa ikitekeleza ahadi zake kuhusiana na makubaliano ya nyuklia ya JCPOA.
Yukiya Amano amesema hayo leo katika siku ya kwanza ya kikao cha 62 cha Baraza Kuu la Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) na kuthibitisha kwamba, Iran imefungamana kikamilifu na suala la utekelezaji wa ahadi zake kuhusu makubaliano ya nyuklia ya Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA).
Amano amesisitiza kuwa, hakuna ishara zozote zinazoonyesha kwamba, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekengeuka au kuhalifu ahadi zake kuhusiana na makubaliano hayo.
Wiki iliyopita pia, Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) ulitoa taarifa mwanzoni mwa kikao cha Bodi ya Magavana ya wakala huo na kusema kwamba, Iran imetekeleza majukumu na ahadi zake zote chini ya makubaliano ya nyuklia ya JCPOA.
Ripoti za mara kwa mara za Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki zimekuwa zikisisitiza kuwa Iran imetekeleza na kuheshimu vipengee vyote vya makubaliano ya nyuklia ya JCPOA yaliyofikiwa baina ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na nchi za kundi la 5+1.
Itakumbukuwa kuwa tarehe 8 Mei mwaka huu rais wa Marekani, Donald Trump aliiondoa nchi hiyo katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, suala ambalo limekumbwa na upinzani mkubwa wa nchi nyingine zilizofanikisha makubaliano hayo ya kimataifa.